The chat will start when you send the first message.
1Ikawa baada ya hayo, Nahashi, mfalme wa wana wa Amoni, akafa, akatawala mwanawe mahali pake.[#2 Sam 10:1; 1 Sam 11:1]
2Naye Daudi akasema, Nitamtendea wema Hanuni, mwana wa Nahashi, kwa kuwa babaye alinitendea mimi wema. Basi Daudi akatuma wajumbe ili kumtuliza kwa habari za babaye. Wakaja watumishi wa Daudi katika nchi ya wana wa Amoni kwa Hanuni, ili wamtulize.
3Lakini wakuu wa wana wa Amoni wakamwambia Hanuni, Je! Unadhani Daudi amewatuma wafariji kwako kwa heshima ya baba yako? Je! Hawakukujia watumishi wake ili kuichunguza nchi, na kuiangamiza, na kuipeleleza?
4Basi Hanuni akawatwaa watumishi wa Daudi, akawanyoa, akawapasulia nguo zao katikati, hadi kiunoni, kisha akawaachilia waondoke.
5Ndipo wakaondoka. Watu walipomwambia Daudi jinsi wajumbe wake walivyotendewa, alituma watu kuwalaki; kwa sababu walikuwa wameaibishwa sana. Mfalme akasema, Ngojeni Yeriko, hadi mtakapoota ndevu zenu, ndipo mrudi.[#Yos 6:24,26; Amu 16:22; 1 Fal 16:34]
6Na wana wa Amoni walipoona ya kuwa wamejisababishia machukizo kwa Daudi, Hanuni na wana wa Amoni wakatuma talanta elfu moja za fedha ili kukodi magari na wapanda farasi kutoka Mesopotamia, na kutoka Atam-maaka, na kutoka Soba.[#1 Sam 14:47; 2 Sam 8:3; 10:6; 1 Fal 11:23; 1 Nya 18:5,9]
7Basi wakakodi magari elfu thelathini na mbili, na mfalme wa Maaka na watu wake; nao walikuja wakatua mbele ya Medeba. Na wana wa Amoni wakakusanyika kutoka miji yao, wakaja vitani.[#Hes 21:30; Yos 13:9; Isa 15:2]
8Basi Daudi aliposikia habari akamtuma Yoabu, na jeshi lote la mashujaa.
9Wakatoka wana wa Amoni, wakajipanga kwa vita langoni pa mji; na hao wafalme waliokuja walikuwa peke yao uwanjani.[#2 Sam 11:1]
10Basi Yoabu alipoona ya kwamba wamejipanga kwa vita juu yake mbele na nyuma, akachagua baadhi ya wateule wote wa Israeli, akawapanga juu ya Washami.
11Na hao watu waliosalia akawatia mikononi mwa Abishai, nduguye, nao wakajipanga juu ya wana wa Amoni.
12Akasema, Washami wakiwa ni hodari mno kwangu, ndipo wewe utanisaidia; lakini wana wa Amoni wakiwa ni hodari mno kwako, ndipo mimi nitakusaidia wewe.
13Kuwa hodari, tuwe na ujasiri, kwa ajili ya watu wetu, na kwa ajili ya miji ya Mungu wetu; naye BWANA afanye yaliyo mema machoni pake.[#Zab 20:7; 34:22; 125:1; Mit 16:3,20; 28:25; Isa 30:18; Yer 17:5-8]
14Basi Yoabu, na watu waliokuwa pamoja naye, wakakaribia kupigana na Washami; nao wakakimbia mbele yake.[#Law 26:7,8; Hes 14:9; Kum 28:7]
15Na wana wa Amoni walipoona ya kwamba Washami wamekimbia, wakakimbia nao mbele ya Abishai, nduguye, wakaingia mjini. Ndipo Yoabu akaja Yerusalemu.
16Na Washami walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, wakatuma wajumbe, wakawaleta Washami walioko ng'ambo ya Mto, na Shobaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri, akawaongoza.[#2 Sam 10:16]
17Alipoambiwa Daudi; akakusanya Israeli wote, akavuka Yordani, akawajia, akapanga vita juu yao. Basi Daudi alipopanga vita juu ya Washami, wakapigana naye.
18Washami wakakimbia mbele ya Israeli; naye Daudi akawaua katika Washami watu wa magari elfu saba, na askari waendao kwa miguu elfu arubaini, akamwua na Shobaki, jemadari wa jeshi.[#Zab 33:16; Mit 21:31]
19Na watumishi wa Hadadezeri walipojiona kuwa wameshindwa mbele ya Israeli, walifanya amani na Daudi, wakamtumikia; wala Washami hawakukubali kuwasaidia wana wa Amoni tena.