The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Daudi akasema, Hii ndiyo nyumba ya BWANA Mungu, na hii ndiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.[#Kum 12:5; 2 Sam 24:18; 1 Nya 21:18-28; 2 Nya 3:1]
2Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu.[#1 Fal 9:21]
3Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyoweza kupimika;[#1 Fal 7:47]
4na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro walimletea Daudi mierezi tele.[#1 Fal 5:6]
5Daudi akasema, Sulemani mwanangu angali ni mchanga bado, na hana uzoefu, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.[#1 Fal 3:7; 1 Nya 29:1]
6Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba.
7Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu.[#2 Sam 7:2; 1 Fal 8:17; 1 Nya 17:1; 28:2; Mdo 7:46; Kum 12:5]
8Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;[#1 Fal 5:3; 1 Nya 28:3]
9tazama, utapata mwana, atakayekuwa mtu wa amani; nami nitampa amani mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake;[#1 Nya 28:5; 1 Fal 4:25; 5:4; #22:9 maana yake ni Mtulivu.]
10huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakiimarisha milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli.[#2 Sam 7:13; 1 Fal 5:5; 1 Nya 17:12; 28:6; Zab 89:26,27; Ebr 1:5]
11Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kuhusu habari zako.[#Rum 8:31]
12BWANA na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike Torati ya BWANA, Mungu wako.[#Kum 4:6; 1 Fal 3:9; Zab 72:1]
13Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, BWANA alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike.[#Yos 1:7; 1 Fal 6:12,13; 9:4,5; 1 Nya 11:9,15; 28:7; Isa 3:10; Kum 31:7; 1 Nya 28:20]
14Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya BWANA, talanta laki moja za dhahabu, na talanta milioni moja za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza.
15Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanya kazi ya mawe na miti, na kila aliye stadi kwa kazi yoyote;
16ya dhahabu, ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, hapana hesabu; basi inuka ushike kazi, naye BWANA na awe pamoja nawe.
17Tena Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli, kwamba wamsaidie Sulemani mwanawe, akisema,
18Je! Si BWANA, Mungu wenu, aliye pamoja nanyi? Na kuwapa amani pande zote? Kwa kuwa wenyeji wa nchi amewatia mkononi mwangu; nayo nchi imetiishwa mbele za BWANA, na mbele ya watu wake.[#Kum 12:10; Yos 22:4; 2 Sam 7:1; 1 Nya 23:25]
19Basi sasa jitieni moyo na nia kumtafuta BWANA, Mungu wenu; inukeni basi, mkamjengee BWANA Mungu mahali patakatifu, ili kulileta sanduku la Agano la BWANA, na vyombo vitakatifu vya Mungu, ndani ya nyumba itakayojengwa kwa ajili ya jina la BWANA.[#2 Nya 20:3; 1 Fal 8:6; 2 Nya 5:7; 6:11]