1 Wakorintho 15

1 Wakorintho 15

Kufufuka kwa Kristo

1Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiria; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama,

2na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiria isipokuwa mliamini bure.

3Kwa maana niliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo Maandiko;[#Isa 53:5-12]

4na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko;[#Zab 16:8-10; Mt 12:40; Mdo 2:24-32; 2 Fal 20:5; Isa 54:7; Hos 6:2; Yon 1:17]

5na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Kumi na Wawili;[#Mt 28:16-17; Mk 16:14; Lk 24:34,36; Yn 20:19]

6baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala;

7baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote;[#Lk 24:50]

8na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.[#Mdo 9:3-6; 1 Kor 9:1]

9Maana mimi ni mdogo katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu nililiudhi kanisa la Mungu.[#Mdo 8:3; Efe 3:8; Mt 5:19; 1 Tim 1:15]

10Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nilizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.[#2 Kor 11:5,23; 6:1]

11Basi kama ni mimi, au kama ni wao, ndivyo tuhubirivyo na ndivyo mlivyoamini.

Kufufuliwa kwa mwili

12Basi, ikiwa Kristo anahubiriwa ya kwamba amefufuka katika wafu, mbona baadhi yenu husema kwamba hakuna kiyama ya wafu?

13Lakini kama hakuna kiyama ya wafu, Kristo naye hakufufuka;

14tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na imani yenu ni bure.

15Naam, na sisi tumeonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu; kwa maana tulimshuhudia Mungu ya kuwa alimfufua Kristo, ambaye hakumfufua, ikiwa wafu hawafufuliwi.[#Mdo 1:22; 5:32]

16Maana kama wafu hawafufuliwi, Kristo naye hakufufuka.[#1 Kor 6:14]

17Na kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu.

18Na hapo wao nao waliolala katika Kristo wamepotea.

19Kama tumemtumaini Kristo katika maisha haya tu, sisi tu watu wa kusikitikiwa ziadi kuliko watu wote.

20Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.[#Kol 1:18; 1 Kor 11:30]

21Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.[#Mwa 3:17-19; Rum 5:12,18]

22Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

23Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.[#1 The 4:16; Ufu 20:5]

24Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu.[#Dan 2:44]

25Maana sharti amiliki yeye, hata awaweke adui zake wote chini ya miguu yake.[#Zab 110:1; Mt 22:44]

26Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.[#Ufu 20:14; 21:4]

27Kwa kuwa, Alivitiisha vitu vyote chini ya miguu yake. Lakini atakaposema, Vyote vimetiishwa, ni dhahiri ya kuwa yeye aliyemtiishia vitu vyote hayumo.[#Zab 8:6]

28Basi, vitu vyote vikiisha kutiishwa chini yake, ndipo Mwana mwenyewe naye atatiishwa chini yake yeye aliyemtiishia vitu vyote, ili kwamba Mungu awe yote katika wote.

29Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?

30Na sisi, kwa nini tumo hatarini kila saa?[#Rum 8:36]

31Naam, ndugu, kwa huku kujisifu kwangu niliko nako juu yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu, ninakufa kila siku.[#2 Kor 4:10,11]

32Ikiwa, kwa jinsi ya kibinadamu, nilipigana na hayawani wakali kule Efeso, nina faida gani? Wasipofufuliwa wafu, na tule, na tunywe, maana kesho tutakufa.[#Isa 22:13]

33Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

34Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.[#Rum 13:11; Efe 5:14; 1 Kor 6:5; Mdo 26:8]

Mwili wa ufufuo

35Lakini labda mtu atasema, Wafu wafufuliwaje? Nao huja kwa mwili gani?

36Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa;[#Yn 12:24]

37nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;

38lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake.[#Mwa 1:11]

39Nyama zote hazifanani; nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki.

40Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.

41Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.

42Hivyo ndivyo ilivyo kwa kiyama ya wafu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutoharibika;

43hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu;[#Flp 3:20,21]

44hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.

45Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa kiumbe aliye hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.[#Mwa 2:7; Yn 6:63; 2 Kor 3:6,17]

46Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.

47Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.[#Mwa 2:7]

48Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.

49Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.[#Mwa 5:3]

50Ndugu zangu, nisemayo ni haya, ya kuwa nyama na damu haziwezi kuurithi ufalme wa Mungu; wala uharibifu kurithi kutoharibika.[#1 Kor 6:13]

51Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,[#1 The 4:15-17]

52kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.[#Mt 24:31; 1 The 4:16]

53Maana sharti huu uharibikao uvae kutoharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.[#2 Kor 5:4]

54Basi huu uharibikao utakapovaa kutoharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa katika ushindi.[#Isa 25:8]

55Kuko wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? Uko wapi, Ewe mauti, uchungu wako?[#Hos 13:14; Isa 25:8]

56Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati.[#Rum 7:13; 6:14]

57Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.

58Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mnajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.[#2 Nya 15:7; Ufu 14:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya