1 Wakorintho 5

1 Wakorintho 5

Uzinzi hulichafua kanisa

1Hakika habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye.[#Kum 22:30; Law 18:7,8]

2Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.

3Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.[#Kol 2:5]

4Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu;[#Mt 16:19; 18:18; 2 Kor 13:10]

5kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu.[#1 Tim 1:20; 1 Pet 4:6]

6Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima?[#Gal 5:9]

7Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;[#Kut 12:5,21; 13:7; Isa 53:7; 1 Pet 1:19]

8basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.[#Kut 13:7; 12:3-20; Kum 16:3]

Uzinzi hauna budi kuhukumiwa

9Niliwaandikia katika barua yangu, kwamba msichangamane na wazinzi.[#Mt 18:17; 2 The 3:14]

10Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang'anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.

11Lakini, mambo yalivyo, niliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang'anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.[#2 The 3:6; Tit 3:10; 2 Yoh 1:10]

12Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje? Ninyi hamwahukumu hao walio ndani?[#Mk 4:11]

13Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu. Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.[#Kum 13:5; 17:7; 22:24]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya