1 Wakorintho 9

1 Wakorintho 9

Haki ya mtume

1Je! Mimi siko huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si kazi yangu katika Bwana?[#1 Kor 15:8; Mdo 26:16; 22:17]

2Kwa maana ikiwa mimi si mtume kwa wengine, lakini ni mtume kwenu ninyi; kwa maana ninyi ndinyi mhuri wa utume wangu katika Bwana.[#2 Kor 3:2,3]

3Hilo ndilo jawabu langu kwa wale wanaoniuliza.

4Je! Hatuna uwezo wa kula na kunywa?[#Lk 10:8]

5Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?[#Yn 1:42]

6Au je! Ni mimi peke yangu na Barnaba tusio na uwezo wa kutofanya kazi?

7Ni askari gani aendaye vitani wakati wowote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?

8Je! Ninanena hayo kwa kibinadamu? Au torati nayo haisemi yayo hayo?

9Kwa maana katika Torati ya Musa imeandikwa, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Je! Hapo Mungu aangalia mambo ya ng'ombe?[#Kum 25:4; 1 Tim 5:18]

10Au yamkini anena hayo kwa ajili yetu? Naam, yaliandikwa kwa ajili yetu; kwa kuwa alimaye nafaka ni haki yake kulima kwa matumaini, naye apuraye nafaka ni haki yake kutumaini kupata sehemu yake.[#2 Tim 2:6]

11Ikiwa sisi tuliwapandia ninyi vitu vya rohoni, je! Ni neno kubwa tukivuna vitu vyenu vya mwilini?[#Rum 15:27]

12Ikiwa wengine wanashiriki uwezo huu juu yenu, sisi si zaidi? Lakini hatukuutumia uwezo huo; bali twayavumilia mambo yote tusije tukaizuia Habari Njema ya Kristo.[#Mdo 20:34,35; 1 Kor 13:7; 2 Kor 11:9]

13Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiayo madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?[#Kum 18:1-3; Hes 18:8,31]

14Na Bwana vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili.[#Mt 10:10; Lk 10:7; Gal 6:6]

15Lakini mimi sikutumia mambo hayo hata moja. Wala siyaandiki hayo ili iwe hivyo kwangu mimi; maana ni heri nife kuliko mtu awaye yote abatilishe huku kujisifu kwangu.[#Mdo 18:3]

16Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili![#Yer 20:9]

17Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili.[#1 Kor 4:1]

18Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa ninapohubiri, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili.[#1 Kor 8:9]

19Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nilijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi.[#Mt 20:26,27]

20Nilikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe siko chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.[#Mdo 16:3; 21:20-26]

21Kwa wale wasio na sheria nilikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria.[#Gal 2:3]

22Kwa wanyonge nilikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.[#2 Kor 11:29; Rum 11:14]

23Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine.

24Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.[#2 Tim 4:7; Flp 3:14]

25Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo ili wapokee taji liharibikayo; bali sisi tupokee taji lisiloharibika.[#2 Tim 2:4,5; 4:8; 1 Pet 5:4; Yak 1:12]

26Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;

27bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiria wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.[#Rum 8:13; 13:14]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya