1 Wafalme 13

1 Wafalme 13

Mtu wa Mungu kutoka Yuda

1Na tazama, akatoka mtu wa Mungu katika Yuda kwa neno la BWANA, akafika Betheli. Naye Yeroboamu alikuwa akisimama penye madhabahu, afukize uvumba.[#2 Fal 23:17; 1 Fal 12:32]

2Basi mtu huyo akapiga kelele juu ya madhabahu, kwa neno la BWANA akasema, Ee madhabahu, madhabahu, BWANA asema hivi, Angalia, mtoto atazaliwa katika nyumba ya Daudi, jina lake Yosia; na juu yako atawatambika makuhani wa mahali pa juu, wanaofukiza uvumba juu yako, na mifupa ya watu itateketezwa juu yako.[#2 Fal 23:15,16]

3Akatoa ishara siku ile ile, akasema, Hii ndiyo ishara aliyoinena BWANA, Tazama, madhabahu itapasuka, na majivu yaliyo juu yake yatamwagika.[#Kut 4:8,9; Kum 13:1,3; 2 Fal 20:8; Isa 7:14; 38:7; Yer 44:29; Yn 2:18; 1 Kor 1:22]

4Ikawa, mfalme Yeroboamu alipoyasikia maneno ya yule mtu wa Mungu, alipopiga kelele juu ya madhabahu huko Betheli, alinyosha mkono wake pale madhabahuni, akasema, Mkamateni. Basi ule mkono wake aliounyosha ukakatika, wala hakuweza kuurudisha kwake tena.[#Yer 20:2; Mdo 12:1; Mit 21:30; Isa 8:9,10; 54:17; Mdo 5:39; 13:8-11; 2 Kor 10:6]

5Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la BWANA.

6Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.[#Kut 8:8; 9:28; 10:17; Hes 21:7; Yer 37:3; Mdo 8:24; Yak 5:16; Kut 8:12; 1 Sam 12:23; Mt 5:44; Mdo 7:60; Rum 12:21]

7Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.[#1 Sam 9:7; 2 Fal 5:15; 1 Kor 2:14]

8Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;[#Hes 22:18; 24:13]

9maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la BWANA, kusema, Usile chakula chochote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.[#1 Kor 5:11; 2 Yoh 1:11]

10Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.

11Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.

12Baba yao akawaambia, Amekwenda zake kwa njia ipi? Kwa maana wanawe walikuwa wameiona njia ile aliyoiendea yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda.

13Akawaambia wanawe, Nitandikieni punda. Wakamtandikia punda, naye akampanda.

14Akamfuata mtu wa Mungu, akamkuta ameketi chini ya mwaloni, akamwambia, Je! Wewe ndiwe yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda? Akamwambia, Mimi ndiye.

15Akamwambia, Karibu kwangu nyumbani, ule chakula.

16Naye akamwambia, Siwezi kurudi pamoja nawe, wala kuingia pamoja nawe; wala sili chakula wala sinywi maji pamoja nawe hapa;

17kwani nimeambiwa kwa neno la BWANA, Usile chakula wala usinywe maji huko, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.[#1 Fal 20:35; 1 The 4:15]

18Akamwambia, Mimi nami ni nabii kama wewe, na malaika akaniambia kwa neno la BWANA, kusema, Mrudishe pamoja nawe nyumbani kwako, ale chakula, akanywe maji. Lakini alisema uongo.[#Yer 5:12; Mt 7:15; 1 Yoh 4:1; Gal 1:8; Yer 29:31,32; Zab 63:11; Mit 6:16,17,19; 30:6; Eze 13:8,9; 1 Tim 4:1,2; 2 Pet 2:18,19]

19Basi mtu yule akarudi pamoja naye, akala chakula, akanywa maji nyumbani mwake.

20Hata ikawa, walipokuwa wameketi mezani, neno la BWANA likamjia nabii yule aliyemrudisha;[#Hes 23:5; Yn 11:51]

21akamlilia yule mtu wa Mungu aliyetoka katika Yuda, akinena, BWANA asema hivi, Kwa sababu umeiasi kauli ya BWANA, wala hukuishika amri ile aliyokuamuru BWANA, Mungu wako,

22bali umerudi, ukala chakula ukanywa maji, hapo alipokuambia, Usile chakula, wala usinywe maji; maiti yako haitaliingia kaburi la baba zako.

23Basi ikawa, alipokwisha kula chakula na kunywa maji, yule nabii aliyemrudisha akamtandikia punda.

24Na alipokuwa amekwenda zake, simba alimkuta njiani, akamwua. Maiti yake ikatupwa njiani, na yule punda akasimama karibu naye; na yule simba naye akasimama karibu na maiti.[#Kum 4:24; 6:15; 1 Fal 20:36; 2 Sam 6:7; 2 Fal 6:24; Mhu 12:13,14; Eze 24:24; Nah 1:2; 1 Pet 4:17]

25Na tazama, watu wakapita, wakauona mzoga umetupwa njiani, na yule simba akisimama karibu na mzoga, wakaenda, wakatoa habari katika mji ule alimokaa yule nabii mzee.

26Na yule nabii aliyemrudisha njiani alipopata habari, akasema; Ndiye yule mtu wa Mungu, aliyeiasi kauli ya BWANA; kwa hiyo BWANA amempambanisha na simba, simba akamrarua, akamwua, sawasawa na neno la BWANA alilomwambia.

27Akawaambia wanawe, akasema, Nitandikieni punda. Wakamtandikia.

28Akaenda, akamwona yule maiti ametupwa njiani, na punda na simba wamesimama karibu na maiti; yule simba alikuwa hakumla maiti, wala hakumrarua punda.[#Law 10:2,5; Ayu 5:22,23; 38:11; Dan 6:22]

29Nabii yule akamtwaa maiti wa yule mtu wa Mungu, akamweka juu ya punda wake, akamrudisha; yule nabii mzee akaenda mjini mwake, kukaa matanga, na kumzika.

30Akamweka maiti katika kaburi lake mwenyewe; wakamlilia, wakisema, Aa! Ndugu yangu![#1 Fal 14:13; Yer 22:18; Mdo 8:2]

31Hata ikawa, alipokwisha kumzika, akawaambia wanawe, akasema, Nikifa mimi, nizikeni katika kaburi hili alimozikwa yule mtu wa Mungu; iwekeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.[#Hes 23:10; Rut 1:17; Zab 26:9; Mhu 8:10]

32Kwa maana neno hilo alilolia juu ya madhabahu katika Betheli, kwa neno la BWANA, na juu ya nyumba zote za mahali pa juu zilizo katika miji ya Samaria, hakika litatimizwa.[#2 Fal 23:16,19; Law 26:30; Hos 12:11; 1 Fal 16:24; 2 Nya 25:13; Yn 4:5; Mdo 8:1,14]

33Baada ya hayo Yeroboamu hakuiacha njia yake mbovu, lakini akafanya tena makuhani wa mahali pa juu, wa watu wowote.[#1 Fal 12:31,32; 2 Nya 13:9; Yer 3:8; Kut 28:41; Amu 17:12; 2 Nya 11:14,15]

34Kila aliyetaka akamweka wakfu, ili wawepo makuhani wa mahali pa juu. Jambo hilo likawa dhambi kwa nyumba ya Yeroboamu, hata kuiharibu, na kuifuta usoni pa nchi.[#1 Fal 12:30; 2 Fal 10:31; 17:20-23; 1 Fal 14:10; 15:29,30]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya