The chat will start when you send the first message.
1Huyo Sulemani akafanya ujamaa na Farao, mfalme wa Misri, akamwoa binti yake Farao, akamleta mjini mwa Daudi, hata alipokwisha kuijenga nyumba yake, na nyumba ya BWANA, na ukuta wa kuuzunguka Yerusalemu.[#1 Fal 9:15]
2Ila watu walikuwa wakitoa dhabihu katika mahali pa juu, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la BWANA, hata siku zile.[#Law 17:3; Kum 12:2; 1 Fal 22:43]
3Sulemani naye akampenda BWANA, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.[#Kum 6:5; 10:12; Zab 31:23; 145:20; Mt 22:37; Mk 12:30; Lk 10:27; Rum 8:28; 1 Kor 8:3; 1 Yoh 5:3; 2 Yoh 1:6]
4Basi mfalme akaenda Gibeoni, ili atoe dhabihu huko; kwa kuwa ndipo mahali pa juu palipo pakuu. Sulemani akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya madhabahu ile.[#1 Nya 16:39]
5Na huko Gibeoni BWANA akamtokea Sulemani katika ndoto ya usiku; Mungu akamwambia, Omba utakalo nikupe.[#1 Fal 9:2; 2 Nya 1:3; Hes 12:6; Mt 1:20; 2:23; Yn 15:7]
6Sulemani akasema, Umemfanyia mtumwa wako Daudi baba yangu fadhili kuu, kadiri alivyoenenda mbele zako katika kweli, na katika haki, na katika unyofu wa moyo pamoja nawe; nawe umemwekea na fadhili hii kubwa, maana umempa mwana wa kuketi kitini pake kama ilivyo leo.[#2 Nya 1:8]
7Na sasa, Ee BWANA, Mungu wangu, umenitawaza niwe mfalme mimi mtumwa wako badala ya Daudi baba yangu; nami ni mtoto mdogo tu; sijui jinsi inipasavyo kutoka wala kuingia.[#1 Nya 29:1; Mhu 10:16; Yer 1:6; Hes 27:17; Ayu 32:6-8]
8Na mtumwa wako yuko katikati ya watu wako uliowachagua, watu wengi wasioweza kuhesabiwa, wala kufahamiwa idadi yao, kwa kuwa ni wengi.[#Kum 7:6; Mwa 13:16; 15:5]
9Kwa hiyo nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya; maana ni nani awezaye kuwahukumu watu hawa wako walio wengi?[#2 Nya 1:10; Zab 72:1; Mit 2:3; 16:16; Yak 1:5; Ebr 5:14]
10Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, ya kuwa Sulemani ameomba neno hili.
11Mungu akamwambia, Kwa kuwa umeomba neno hili, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; wala hukutaka utajiri kwa nafsi yako; wala hukutaka roho za adui zako; bali umejitakia akili za kujua kuhukumu;[#Yak 4:3]
12basi, tazama, nimefanya kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wa hekima na wa akili; hata kabla yako hapakuwa na mtu kama wewe, wala baada yako hatainuka mtu kama wewe.[#1 Yoh 5:14; 1 Fal 4:29; 5:12; 10:23,24; Mit 3:13-18; 8:1-36; Mhu 1:16]
13Na mambo yale usiyoyaomba nimekupa, mali na fahari, hata hapatakuwa na mtu katika wafalme kama wewe, siku zako zote.[#Mt 6:33; Efe 3:20; 1 Fal 4:21,24; 10:23; Mit 3:16; 1 Kor 3:21-23]
14Nawe ukienda katika njia zangu, na kuyashika mausia yangu, na amri zangu, kama baba yako Daudi alivyokwenda, basi nitazifanya siku zako kuwa nyingi.[#Zab 91:16; Mit 3:2]
15Naye Sulemani akaamka, na kumbe! Ni ndoto. Akaenda Yerusalemu, akasimama mbele ya sanduku la Agano la BWANA, akatoa sadaka za kuteketezwa, akatoa na sadaka za amani; akawafanyia karamu watumishi wake wote.[#Mwa 41:7; Yer 31:26; Mwa 31:54; 40:20; 1 Fal 8:65; Est 1:3; Dan 5:1; Mk 6:21]
16Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.[#Law 19:29; Kum 23:17; Hes 27:2]
17Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nilizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.
18Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.
19Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia.
20Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.
21Nilipoamka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe. Amekufa. Na asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa.
22Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.
23Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.
24Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.
25Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.
26Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.[#Mwa 43:30; Isa 49:15; Yer 31:20; Hos 11:8]
27Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.
28Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.[#Ezr 7:25; Mhu 7:19; Isa 11:3; Dan 1:17; 5:11; Kol 2:2,3]