1 Wamakabayo 1

1 Wamakabayo 1

UTANGULIZI

Iskanda Mkuu

1Ikawa Iskanda wa Makedonia, mwana wa Filipo, alitoka katika nchi ya Kitimu akampiga Dario, mfalme wa Waajemi na Wamedi, na baada ya kumpiga alitawala mahali pake.

2Akapiga vita vingi, akatwaa ngome nyingi, akawaua Wafalme.

3Akaendelea hata kwenye miisho ya nchi, akateka mataifa mengi. Lakini nchi yote ilipotiishwa mbele yake alitukuka, na moyo wake uliinuka.

4Akaunda jeshi kubwa mno, akamiliki nchi na mataifa na wakuu na kuwatoza ushuru.

5Baada ya hayo alishikwa na ugonjwa, akajua ya kuwa yu karibu kufa.

6Akawaita watumishi wake, watu wastahiki waliolelewa pamoja naye tangu ujana wake, akawagawia milki yake alipokuwa angali hai.

7Naye Iskanda alikuwa ametawala miaka kumi na miwili kabla ya kufa kwake.

8Watumishi wake wakatawala, kila mmoja katika nchi yake.

9Baada ya kufa kwake wakajitia taji, na wana wao baada yao, kwa miaka mingi. Wakafanya mabaya mengi duniani.

Antioko Epifani atawazwa na kuingizwa kwa ustaarabu wa Kigiriki katika Israeli

10Katika hao kulichipuka chipukizi lenye dhambi, ndiye Antioko Epifani, mwana wa mfalme Antioko, ambaye alikuwa amewekwa amana kwa Warumi. Naye alitawazwa katika mwaka wa mia thelathini na saba wa enzi ya Wagiriki.[#2 Mak 4:7]

11Siku zile walitokea wavunja sheria katika Israeli, wakashawishi wengi, wakisema, Twende tufanye maagano na mataifa wanaotuzunguka, maana tangu tulipofarakana nao misiba mingi imetupata.

12Jambo hilo likapendeza machoni pao,

13hata watu fulani wakafanya hima kwenda kwa mfalme, naye akawapa ruhusa kuzifuata kawaida za mataifa.

14Wakafanya kiwanja cha michezo Yerusalemu kama kawaida ya mataifa,

15wakajifanya kana kwamba hawakutahiriwa wakajitenga na agano takatifu. Hivyo walijiunga na mataifa na kujiuza wafanye uovu.[#1 Kor 7:18]

ANTIOKO EPIFANI ANATEKA NYARA HEKALU NA KUWADHULUMU WACHAJI WA TORATI

Antioko katika Misri

16Antioko alipoona ufalme wake umetengemaa vema alikusudia kuitawala Misri pia ili kuzimiliki falme mbili.

17Akaingilia Misri na jeshi kubwa, na magari, na tembo, na wapanda farasi, na vyombo vingi sana.

18Akafanya vita juu ya Tolemayo, mfalme wa Misri, naye Tolemayo alirejea nyuma mbele yake, akakimbia, na wengi walianguka wametiwa jeraha za mauti.

19Akaikamata miji yenye maboma katika nchi ya Misri, akateka Misri nyara.

Wayahudi wateswa

20Basi, Antioko akiisha kuishinda Misri katika mwaka wa mia arubaini na tatu alirudi, akaiendea Israeli akafika Yerusalemu na jeshi kubwa.

21Akaingia katika hekalu kwa jeuri, akachukua madhabahu ya dhahabu, na kinara cha taa na vyombo vyake vyote,

22na meza ya mikate ya wonyesho, na vikombe na mabakuli, na vyetezo vya dhahabu, na pazia, na taji, na kuyaambua mapambo ya dhahabu katika ukuta.

23Akavitwaa vyombo vya fedha na dhahabu na vyombo vya thamani, na vitu vyote vilivyo tunu alivyoweza kuviona.

24Hata akiisha kuvitwaa vyote, aliondoka akarudi kwake. Aliua watu wengine, na kutoa maneno ya jeuri.

25Kukatokea kilio kikubwa katika Israeli, kila mahali;

26Wakuu na wazee waliugua,

Wasichana na wavulana walihuzunika,

Na uzuri wa wanawake ulitoweka.

27Kila bwana arusi aliomboleza,

Na bibi chumbani mwa bibi arusi alilia;

28Nchi ilitetemeka kwa ajili ya wenyeji wake,

Na nyumba yote ya Yakobo ilivikwa fedheha.

Kutawazwa dini za mataifa

29Baada ya miaka miwili mfalme alipeleka mtoza ushuru mkuu kwenye miji ya Uyahudi, akaja Yerusalemu na askari wengi.

30Akawadanganya kwa maneno ya amani, wakamwamini. Lakini aliuangukia mji kwa ghafla akaupiga pigo kubwa, akawaharibu watu wengi wa Israeli.

31Aliuteka mji akauchoma moto, akazibomoa nyumba zake na kuta zake pande zote.

32Wakawachukua wanawake na watoto utumwani, na kuwakamata ng'ombe.

33Wakauzungusha mji wa Daudi ukuta mkubwa, imara, wenye minara ya nguvu, ukawa ngome yao.

34Wakakalisha humo taifa lenye dhambi, wasioishika sheria, wakajiimarisha humo.

35Wakaweka akiba ya silaha na chakula, wakachukua nyara zote za Yerusalemu wakaziweka humo.

36Ikawa hatari kubwa, mahali pa kuliotea hekalu, adui mbaya kwa Israeli sikuzote.

37Walimwaga damu isiyo na hatia pande zote za patakatifu,

Wakalinajisi hekalu

38Wenyeji wa Yerusalemu walikimbia kwa sababu yao,

Mji ukawa makao ya wageni,

Mji wa kigeni kwa wazaliwa wake,

Ulioachwa na watoto wake,

39Patakatifu pake palifanywa ukiwa kama jangwa,

Sikukuu zake zikageuka kuwa kilio,

Sabato zake lawama,

Na heshima yake dharau.

40Utukufu wake ulivyokuwa mwingi

Ndivyo aibu yake ilivyoongezeka,

Na ukuu wake uligeuka maombolezo.

41Mfalme Antioko akaziandikia milki zake zote, kwamba wote wawe taifa moja,

42kila mtu aache sheria zake za asili. Watu wote wa mataifa wakaikubali amri ya mfalme,

43hata wengi katika Israeli walifuata ibada yake, wakitoa dhabihu kwa miungu ya uongo na kutia unajisi Sabato.

44Mfalme akapeleka barua Yerusalemu na kwenye miji ya Uyahudi kwamba wazifuate desturi zilizo za kigeni kwao;

45waache kutoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu na sadaka ya kinywaji hekaluni; wazinajisi Sabato na sikukuu;

46na kulitia unajisi hekalu na waliotakasika.

47Tena, wajenge madhabahu na mahekalu na viwanja vitakatifu vya miungu ya uongo, na kutoa dhabihu za nguruwe na wanyama wachafu;

48waache wana wao bila kutahiriwa, na kujitia nafsi zao unajisi kwa uchafu na ukafiri wa kila namna;

49kusudi waisahau sheria na kuzibadili kawaida zao.

50Naye asiye litii neno la mfalme atakufa.

51Kwa maneno hayo aliwaandikia wote wa milki yake, akaweka wasimamizi juu ya watu wote, na kuwaamuru watu wa miji yote watoe dhabihu mijini mwao.

52Wengi wakajiunga nao, yaani wao waliokuwa wameiasi sheria; wakafanya maovu katika nchi,

53hata Waisraeli walilazimika wajifiche katika makimbilio ya siri huku na huko.

54Siku ya ishirini na tano ya Kislevu, mwaka wa mia arubaini na tano, waliweka chukizo la uharibifu juu ya madhabahu,[#Dan 9:27; 11:31; 12:11; 1 Mak 6:7; Mt 24:15; Mk 13:14]

55na katika miji ya Uyahudi kila upande walijenga vimadhabahu vya miungu, wakafukiza uvumba milangoni pa nyumba na njiani.

56Na vitabu vya sheria walivyovipata walivirarua vipande vipande wakaviteketeza.

57Mtu yeyote aliyepatikana na kitabu, au aliyeonekana anaifuata sheria, alihukumiwa kufa kama alivyoamuru mfalme.

58Hivyo ndivyo walivyowatenda Waisraeli kwa jeuri, wale walioonekana mwezi kwa mwezi katika miji.

59Na siku ya ishirini na tano ya mwezi walitoa dhabihu katika kimadhabahu kilichowekwa juu ya madhabahu.

60Nao wanawake waliowatahiri watoto wao waliwaua kama ilivyoamriwa,[#2 Mak 6:10]

61wakatungika wana wao shingoni mwao; wakawaua wote wa nyumbani mwao, na wale waliowatahiri watoto.

62Hata hivyo wengi katika Israeli walikaza nia zao kwa uthabiti wasile vitu vilivyo najisi.

63Waliona afadhali kufa kuliko kutiwa unajisi kwa vyakula au kulivunja agano takatifu. Wakafa.

64Kukawa hasira kuu juu ya Israeli.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya