The chat will start when you send the first message.
1Yohana akapanda kutoka Gazara, akamweleza baba yake Simoni mambo anayoyafanya Kendebayo.
2Simoni akawaita wanawe wawili wakubwa akawaambia, Mimi na ndugu zangu, na nyumba ya baba yangu, tumepigana vita vya Israeli tangu ujana wetu hata leo. Mambo yamefanikiwa mikononi mwetu hata tumeweza kuiokoa Israeli mara nyingi.
3Lakini mimi sasa ni mzee, nanyi kwa rehema zake mna umri wa kutosha. Mwe, basi, badala ya mimi na ndugu zangu; ondokeni mkalipiganie taifa letu, na msaada utokao mbinguni uwe nanyi.
4Akachagua watu wa nchi elfu ishirini hodari wa vita, na wapanda farasi wakaenda kupigana na Kendebayo, wakalala Modini.
5Wakaondoka asubuhi wakafika uwandani, wakaona jeshi kubwa linakuja kupigana nao, askari na wapanda farasi pia. Kati ya majeshi kulikuwa na mto.
6Yeye na jeshi lake wakajipanga kuwaelekea. Akaona ya kuwa watu wanaogopa kuuvuka mto, basi, alitangulia kuvuka yeye, na watu wake walipomwona walimfuata.
7Akawatenga mafungu mawili akawaweka wapanda farasi katikati, kwa sababu wapanda farasi wa adui walikuwa wengi mno;
8wakapiga tarumbeta. Kendebayo na jeshi lake wakashindwa, wengi wao wakaanguka, wametiwa jeraha, na waliosalia walikimbilia bomani.
9Wakati huo Yuda, ndugu ya Yohana, alijeruhiwa, lakini Yohana aliwafuatia hata kufika Kedroni aliyoijenga Kendebayo.
10Wakaikimbilia minara katika pori la Ashdodi, akaitia moto, wakaanguka watu wapatao elfu mbili. Akarejea Uyahudi kwa amani.
11Tolemayo mwana wa Abubo alikuwa amewekwa jemadari juu ya nchi tambarare ya Yeriko. Alikuwa na fedha na dhahabu nyingi,
12maana alikuwa mkwe wa kuhani mkuu.
13Moyo wake uliinuka, akataka kujifanya mkuu wa nchi, akafanya mashauri ya hila juu ya Simoni na wanawe ili awaondolee mbali.
14Basi, Simoni alikuwa akiikagua miji ya nchi akiangalia matengenezo yake. Akashukia Yeriko, yeye na wanawe Matathia na Yuda, mwaka wa mia moja sabini na saba, mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati.
15Mwana wa Abubo akawapokea kwa ujanja katika ngome ndogo iliyoitwa Doki, aliyoijenga, akawafanyia karamu kubwa, akaficha watu humo ngomeni.
16Simoni na wanawe walipokwisha kunywa sana, Tolemayo na watu wake wakaondoka wakashika silaha zao wakamshambulia Simoni katika chumba cha karamu wakamwua pamoja na wanawe wawili na watumsihi wake wengine.
17Hivyo alitenda jambo la uhaini kabisa, akirudisha mabaya kwa mema.
18Tolemayo akaandika habari za mambo hayo akazipeleka kwa mfalme, akimwomba amletee askari wa kumsaidia, naye atamtolea nchi yao na miji yao.
19Akapeleka watu wengine Gazara kumwua Yohana. Akapeleka barua kwa maamiri wa vikosi kuwaalika kwake awape fedha na dhahabu na tunu.
20Na watu wengine aliwatuma kuishika Yerusalemu na mlima wa hekalu.
21Lakini mtu mmoja alipiga mbio akafika Gazara kabla ya watu hao hawajafika, akamwambia Yohana kwamba baba yake na ndugu zake wameuawa, akasema, Ametuma watu kukuua na wewe pia.
22Aliposikia hayo alifadhaika sana; akawakamata wale watu waliokuja kumwangamiza, akawaua, kwa sababu aliambiwa kuwa wanatafuta kumwua.
23Habari nyingine za Yohana, za vita vyake na matendo yake ya ushujaa, na za majenzi ya kuta alizozijenga, na za kazi zake,
24zimeandikwa katika Kitabu cha Tarehe cha ukuhani wake, tangu wakati alipofanywa kuhani mkuu baada ya baba yake.