1 Petro 3

1 Petro 3

Wake na waume

1Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;[#Efe 5:22; Kol 3:18; Tit 2:5]

2wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.[#1 Pet 2:12]

3Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;[#1 Tim 2:9; Isa 3:18-24]

4bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

5Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.

6Kama vile Sara alivyomtii Abrahamu, akamwita bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, pasipo kutishwa na hofu yoyote.[#Mwa 18:12; Mit 3:25]

7Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu; maana wao pia ni warithi wa neema ya uzima, ili maombi yenu yasizuiliwe na chochote.[#Efe 5:25; Kol 3:19]

Mateso kwa ajili ya kutenda Haki

8Neno la mwisho ni hili; muwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu;[#Rum 12:16]

9watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.[#Zab 34:12-16; Yak 1:26; Mt 5:44; 1 The 5:15; 1 Pet 2:23]

10Kwa maana,[#Zab 34:12-16; Yak 1:26]

Atakaye kupenda maisha,

Na kuona siku njema,

Auzuie ulimi wake usinene mabaya,

Na midomo yake isiseme uongo.

11Na aache mabaya, atende mema;

Atafute amani, aifuate sana.

12Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,

Na masikio yake husikiliza maombi yao;

Bali uso wa Bwana uko juu ya watenda mabaya.

13Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?

14Lakini hata mkiteswa kwa sababu ya kutenda haki, mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu.[#Mt 5:10; Isa 8:12-13; 1 Pet 2:20]

15Muwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa heshima.[#Isa 8:13; Kol 4:6; 1 Pet 1:3,13]

16Nanyi muwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo.[#1 Pet 2:12]

17Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.[#1 Pet 2:20-24]

18Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; akauawa kimwili, lakini akahuishwa kiroho,[#Rum 6:10; Efe 2:18; Ebr 9:28; 10:10]

19ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiria;[#1 Pet 4:8]

20watu wasiotii hapo zamani, wakati Mungu alipowavumilia kwa subira, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji.[#Mwa 6:1—7:7,17,24]

21Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo.[#Efe 5:26; Ebr 10:22]

22Naye yuko katika mkono wa kulia wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.[#Efe 1:20,21; Zab 110:1; Kol 1:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya