The chat will start when you send the first message.
1Sauli alikuwa na umri wa miaka kadha wa kadha hapo alipoanza kutawala; naye akatawala miaka kadha wa kadha juu ya Israeli.[#13:1 Hakuna hakika yoyote ya miaka hiyo kuwa ni mingapi.; #13:1 Hakuna hakika yoyote ya miaka hiyo kuwa ni mingapi.]
2Naye Sauli alijichagulia watu elfu tatu wa Israeli; ambao katika hao, elfu mbili walikuwa pamoja na Sauli katika Mikmashi, na katika mlima wa Betheli na elfu moja pamoja na Yonathani katika Gibea ya Benyamini; nao wale watu waliosalia akawaruhusu waende kila mtu hemani kwake.
3Yonathani akaipiga hiyo ngome ya Wafilisti, iliyokuwako huko Gibea, nao Wafilisti wakapata habari. Naye Sauli akapiga tarumbeta katika nchi yote, huku akisema, Na wasikie Waebrania.[#1 Sam 10:5; Mwa 34:30]
4Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa makuruhi kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali.
5Nao Wafilisti wakakusanyika ili wapigane na Waisraeli, magari elfu thelathini, na wapanda farasi elfu sita, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni.[#Yos 18:12]
6Hata Waisraeli walipoona ya kuwa wako katika dhiki, (maana watu walifadhaishwa), ndipo hao watu wakajificha katika mapango, na katika vichaka, na katika miamba, na katika mashimo, na katika mabirika.[#Amu 6:2]
7Hata baadhi ya Waebrania walivuka Yordani, wakaingia nchi ya Gadi na Gileadi; lakini Sauli alikuwa angali huko Gilgali, nao watu wote wakamfuata wakitetemeka.
8Akangoja siku saba, kwa kadiri ya muda uliowekwa na Samweli lakini Samweli hakuja Gilgali; na hao watu wakatawanyika mbali naye.[#1 Sam 10:8]
9Sauli akasema, Nileteeni hapa sadaka ya kuteketezwa na sadaka za amani. Akaitoa sadaka ya kuteketezwa.[#Kum 12:5-14; 1 Sam 15:22; 1 Fal 3:4; 2 Nya 26:16; Mit 15:8; 21:3,27; Ebr 5:4]
10Hata mara alipokwisha kuitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, kumbe! Samweli akatokea. Naye Sauli akatoka kwenda kumlaki na kumsalimu.[#Rut 2:4]
11Samweli akasema, Umefanya nini? Naye Sauli akasema, Ni kwa sababu niliona ya kuwa watu wanatawanyika mbali nami, na wewe hukuja siku zile zilizonenwa; nao Wafilisti wamekusanyika pamoja huko Mikmashi;
12basi nikasema, Wafilisti watanishukia sasa mpaka Gilgali, kabla sijaomba fadhili za BWANA; kwa hiyo nilijishurutisha, nikatoa sadaka ya kuteketezwa.
13Naye Samweli akamwambia Sauli, Umefanya upumbavu; hukuishika amri ya BWANA, Mungu wako, aliyokuamuru; kwa maana BWANA angaliufanya ufalme wako kuwa imara juu ya Israeli milele.[#2 Sam 12:7-9; 1 Fal 18:18; 2 Nya 16:9; Ayu 34:18; Mit 19:3; Mt 14:3,4; 1 Sam 15:11; Law 17:1; Hes 18:7]
14Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru.[#Mdo 13:22; 1 Sam 2:30; 15:28; 2 Sam 7:15; Zab 78:70; 89:20]
15Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wakawa kama mia sita.[#1 Sam 14:2]
16Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi.
17Nao watekaji wa nyara wakatoka katika kambi ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali;[#Yos 18:23]
18na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika.[#Yos 16:3; 18:13; 1 Nya 6:68; 2 Nya 8:5]
19Basi, hakukuwa mhunzi yeyote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajitengenezea panga au mikuki;[#2 Fal 24:14; Yer 24:1]
20lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake;
21Na walilipa theluthi mbili za shekeli kunoa jembe na miundu, na theluthi moja ya shekeli kunoa mashoka na kuchonga michokoo.
22Hivyo ikawa, siku ya vita, haukuonekana mkononi mwa mtu yeyote, miongoni mwa watu waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani, upanga wala mkuki; isipokuwa Sauli mwenyewe na mwanawe Yonathani walikuwa navyo.[#Amu 3:31; 5:8; 1 Sam 17:47,50; Zek 4:6]
23Na jeshi la Wafilisti wakatoka hata mpito ya Mikmashi.[#1 Sam 14:5; Isa 10:28]