1 Samweli 16

1 Samweli 16

Daudi apakwa mafuta kuwa mfalme

1BWANA akamwambia Samweli, utamlilia Sauli hadi lini, kwa kuwa mimi nimemkataa asiwatawale Waisraeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakutuma kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe.[#2 Fal 9:1; Zab 78:70; Mdo 13:22]

2Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi BWANA akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea BWANA dhabihu.[#1 Sam 20:29]

3Umwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakayotenda; nawe utampaka mafuta yule nitakayemtaja kwako.[#Kut 4:15; 1 Sam 9:16]

4Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani?[#1 Sam 21:1; 2 Sam 6:9; 1 Fal 17:18; Hos 6:5; 11:10; Lk 5:8; 8:37; Mdo 24:25; 1 Fal 2:13; 2 Fal 9:22]

5Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu.[#Kut 19:10]

6Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake.[#1 Fal 12:26; #16:6 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]

7Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.[#Zab 147:10; Isa 55:8; 2 Kor 10:7; 1 Fal 8:39; 1 Nya 28:9; 2 Nya 16:9; Zab 7:9; Yer 11:20; 17:10; Mdo 1:24; Ufu 2:23]

8Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu.

9Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, Wala BWANA hakumchagua huyu.

10Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa.

11Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hadi atakapokuja huku.[#1 Sam 17:12; 2 Sam 7:8; Zab 78:70]

12Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye.[#Wim 5:10; 1 Sam 9:17]

13Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na Roho ya BWANA ikamjia Daudi kwa nguvu kuanzia siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.[#Zab 89:20; Hes 27:18; Amu 11:29; 13:25; 14:6]

Daudi ampigia Sauli kinubi

14Basi, Roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua.[#1 Sam 18:12; Amu 16:20; Zab 51:11; Amu 9:23; 1 Sam 19:9; Isa 19:14]

15Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua.

16Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona.

17Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mniletee.

18Ndipo mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mtoto mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yuko pamoja naye.

19Basi Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese akasema, Mtume Daudi mwanao kwangu, aliye pamoja na kondoo.

20Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe.

21Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akawa mtu wa kumchukulia silaha zake.[#Mwa 41:46; 1 Fal 10:8; Mit 22:29]

22Kisha Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu.

23Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjia Sauli, ndipo Daudi alipokishika kinubi na kukipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya