The chat will start when you send the first message.
1Basi hao Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki; nao Waisraeli wakafanya kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli.[#1 Sam 28:1; 4:1; Yos 19:30; 1 Fal 20:30]
2Nao wakuu wa Wafilisti wakapita mbele, mamia, na maelfu; naye Daudi na watu wake wakapita wa mwisho pamoja na Akishi.[#1 Sam 28:1,2]
3Ndipo wakuu wa Wafilisti wakasema, Waebrania hawa wanafanya nini hapa? Naye Akishi akawaambia wakuu wa Wafilisti, Je! Siye huyu Daudi, yule mtumishi wa Sauli, mfalme wa Israeli, ambaye amefuatana na mimi siku hizi, naam, miaka hii, wala mimi nisione hatia kwake, tangu hapo aliponiangukia mimi hata leo?[#1 Sam 27:7; Dan 6:5; Yn 19:6; 1 Pet 3:16]
4Lakini wakuu wa Wafilisti wakamkasirikia, na kumwambia, Mrudishe huyu, apate kurejea mahali pake ulipomwagiza, wala asiende pamoja nasi vitani, asije akawa adui wetu vitani; kwani mtu huyu angejipatanisha na bwana wake kwa njia gani? Je! Si kwa vichwa vya watu hawa?[#1 Nya 12:19; 1 Sam 14:21]
5Je! Siye huyo Daudi, ambaye waliimbiana habari zake katika michezo, wakisema,[#1 Sam 18:7; 21:12; Mit 27:14]
Sauli amewaua elfu zake,
Na Daudi makumi elfu yake?
6Ndipo Akishi akamwita Daudi, akamwambia, Aishivyo BWANA, wewe umekuwa mwenye adili, tena kutoka kwako na kuingia kwako pamoja nami katika jeshi ni kwema machoni pangu; kwa sababu mimi sikuona uovu ndani yako tangu siku ile uliponijia hata leo; walakini hao wakuu hawakuridhii.[#Hes 27:17; 2 Sam 3:25; 2 Fal 19:27; Zab 121:8; Isa 37:28]
7Basi sasa rudi, uende zako kwa amani, ili usiwachukize hao wakuu wa Wafilisti.
8Naye Daudi akamwambia Akishi, Lakini mimi nimefanyaje? Nawe umeona nini kwangu mimi mtumishi wako, muda wote niliokaa mbele yako hata leo, nisipate ruhusa niende na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?
9Akishi akajibu, akamwambia Daudi, Mimi najua ya kuwa u mwema machoni pangu, kama malaika wa Mungu; ila hao wakuu wa Wafilisti wamesema, Huyu hatakwea pamoja nasi kwenda vitani.[#2 Sam 14:17; 19:27]
10Kwa hiyo sasa amka asubuhi na mapema, wewe na watumishi wa bwana wako waliokuja pamoja nawe; nanyi mtakapoamka asubuhi na mapema, na kupata mwanga, nendeni zenu.
11Basi Daudi akaamka asubuhi na mapema, yeye na watu wake, kwenda zao asubuhi, kuirudia nchi ya Wafilisti. Nao Wafilisti wakakwea kwenda Yezreeli.[#Zab 37:23; 73:2; Mit 16:9; 20:24; Isa 30:21; Yer 10:23; 1 Kor 10:13; 2 Sam 4:4]