1 Samweli 30

1 Samweli 30

Daudi alipiza kuharibiwa kwa Siklagi

1Ikawa, Daudi na watu wake walipokuwa wamefika Siklagi siku ya tatu, hao Waamaleki walikuwa wameshambulia Negebu, na Siklagi, nao wameupiga Siklagi, na kuuchoma moto;[#Kut 17:8-16; Hes 24:20; Kum 25:17,19; 1 Sam 27:8; 28:18; 1 Nya 4:43; Eze 25:15]

2nao wamewachukua mateka wanawake waliokuwamo wakubwa kwa wadogo; hawakuwaua wowote, ila wakawachukua, wakaenda zao.[#Ayu 38:11; Zab 76:10; 89:9; Isa 27:8; Hab 3:2]

3Basi Daudi na watu wake walipoufikia mji, tazama, ulikuwa umechomwa moto; na wake zao, na watoto wao, wanaume kwa wanawake, wamechukuliwa mateka.

4Ndipo Daudi na watu waliokuwa pamoja naye wakapaza sauti zao na kulia, hadi walipokuwa hawana nguvu za kulia tena.[#Hes 14:1]

5Na hao wake wawili wa Daudi walikuwa wamechukuliwa mateka, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, aliyekuwa mkewe Nabali, wa Karmeli.[#1 Sam 25:42-43; 2 Sam 2:2]

6Naye Daudi akafadhaika sana; kwa sababu watu walikuwa wakisema kwamba apigwe kwa mawe, kwa maana hao watu wote walisononeka, kila mtu kwa ajili ya wanawe na binti zake; lakini Daudi alijitia nguvu katika BWANA, Mungu wake.[#Kut 17:4; Yn 8:59; Amu 18:25; 2 Sam 17:8; Zab 31:24; 33:18; 39:7; Yer 17:7,17; Yoe 3:16; Rum 4:20]

7Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.[#1 Sam 22:20-23; 23:6,9]

8Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.[#1 Sam 23:2,4; Zab 22:4,5; 28:6]

9Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye, nao wakakifikia kijito Besori, ambapo wale walioachwa nyuma walikaa.

10Lakini Daudi akaendelea kuwafuatilia, yeye na watu mia nne; kwa maana watu mia mbili walikaa nyuma, ambao walitaka kuzimia hata hawakuweza kukivuka hicho kijito Besori.

11Nao wakamkuta Mmisri nyikani wakamleta kwa Daudi, na kumpa chakula, naye akala; nao wakampa maji ya kunywa;[#Zab 111:2; Mit 3:5,6]

12kisha wakampa kipande cha mkate wa tini, na vishada viwili vya zabibu; naye akiisha kula roho yake ikamrudia; kwa maana hakuwa amekula chakula wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.[#Amu 15:19; 1 Sam 14:27]

13Ndipo Daudi akamwuliza, Wewe ni mtu wa nani; na umetoka wapi? Naye akasema, Mimi ni kijana wa Misri, mtumishi wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu tangu siku hizi tatu nilishikwa na ugonjwa.

14Sisi tulishambulia Negebu ya Wakerethi, na ya milki ya Yuda, na Negebu ya Kalebu; na huo mji wa Siklagi tukauchoma moto.[#2 Sam 8:18; 1 Fal 1:38,44; Eze 25:16; Sef 2:5; Yos 14:13; 15:13]

15Daudi akamwambia, Je! Wewe utaniongoza chini hadi nilifikie jeshi hilo? Naye akasema, Uniapie kwa Mungu, ya kwamba hutaniua, wala kunitia mikononi mwa huyo bwana wangu, nami nitakuongoza chini hata kulifikia jeshi hilo.

16Na hapo alipokuwa amewaongoza chini, tazama, hao walikuwa wametawanyika juu ya nchi yote, wakila na kunywa, na kufanya karamu, kwa sababu ya hizo nyara kubwa walizochukua katika nchi ya Wafilisti, na katika nchi ya Yuda.[#Kut 32:6; 1 Sam 25:36-38; 2 Sam 13:28; Dan 5:1-4; Lk 12:19,20; 21:34; 1 The 5:3; Ufu 11:10,13]

17Naye Daudi akawapiga tangu ukungu wa jioni hadi jioni ya siku ya pili; hakuna aliyeokoka, ila vijana mia nne waliopanda ngamia na kukimbia.[#Ayu 20:5]

18Daudi akawapokonya wote waliokuwa wamechukuliwa na Waamaleki; naye Daudi akawaokoa wakeze wawili.[#Mwa 14:16; Zab 34:9]

19Wala hawakupotewa na kitu, mdogo wala mkubwa, wana wala binti, nyara wala chochote walichojitwalia hao; Daudi akavirudisha vyote.

20Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng'ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.

21Kisha Daudi aliwafikia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.[#Amu 18:15]

22Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu chochote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.[#Kum 13:13; Amu 19:22; 1 Sam 22:2; 25:17; 1 Fal 21:10]

23Ndipo Daudi akasema, La, ndugu zangu, msitende hivyo katika hizo nyara alizotupa BWANA, ambaye ndiye aliyetuhifadhi, akalitia mikononi mwetu lile jeshi lililokuja kinyume chetu.

24Tena ni nani atakayewasikiliza ninyi katika jambo hili? Kwa kuwa kama lilivyo fungu lake yeye ashukaye vitani, ndivyo litakavyokuwa na fungu lake huyo akaaye karibu na vyombo; watagawiwa sawasawa.[#Hes 31:27; Yos 22:8; Zab 68:12]

25Basi ikawa hivyo tangu siku ile na baadaye; akaiweka iwe amri na agizo la Israeli hata leo.

26Basi Daudi alipofika Siklagi, aliwapelekea wazee wa Yuda, rafiki zake, sehemu ya nyara, akasema, Angalieni, zawadi yenu katika nyara za adui za BWANA;

27yaani, kwa hao wa Betheli, na kwa hao wa Ramoth-Negebu, na kwa hao wa Yatiri;[#Mwa 12:8; Yos 19:8; 15:48]

28na kwa hao wa Aroeri, na kwa hao wa Sifmothi, na kwa hao wa Eshtemoa;[#Yos 13:16; 15:50]

29na kwa hao wa Rakali, na kwa hao wa miji ya Wayerameeli, na kwa hao wa miji ya Wakeni;[#1 Sam 27:10; Amu 1:16]

30na kwa hao wa Horma, na kwa hao wa Korashani, na kwa hao wa Athaki;[#Amu 1:17]

31na kwa hao wa Hebroni, na kwa hao wa kila mahali alipotembelea Daudi mwenyewe na watu wake.[#Yos 14:13; 2 Sam 2:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya