1 Samweli 9

1 Samweli 9

Sauli ateuliwa kuwa mfalme

1Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.[#1 Sam 14:51; 1 Nya 8:33; 9:39; Mdo 13:21]

2Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.[#1 Sam 10:23]

3Na punda wa Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, chukua mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao.

4Naye akapita katika nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita katika nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita katika nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita katika nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata.[#2 Fal 4:42]

5Walipofika katika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Hebu turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi.[#1 Sam 1:1]

6Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu anaheshimiwa; yote asemayo hutukia hakika; basi, twende huko; labda yeye anaweza kutuambia kuhusu safari yetu tunayoiendea.[#Kum 33:1; 1 Sam 2:27; 1 Fal 13:1; 2 Fal 6:6; 1 Tim 6:11; 1 Sam 3:19; Isa 44:26; Mt 24:35]

7Ndipo Sauli akamwambia mtumishi wake, Lakini tukienda, tumpelekee mtu huyo kitu gani? Maana chakula kimekwisha vyomboni mwetu, wala hapana zawadi ya kumpelekea mtu wa Mungu; tuna nini sisi?[#Amu 6:18; 13:17; 1 Fal 14:3; 2 Fal 4:42; 8:8]

8Yule mtumishi akamjibu Sauli, akasema, Tazama, mkononi mwangu nina fedha robo ya shekeli; nitampa huyo mtu wa Mungu fedha hiyo, atuambie njia yetu.

9(Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.)[#Mwa 25:22; Kut 28:30; Hes 27:21; Amu 1:1; 20:18-28; 2 Sam 24:11; 2 Fal 17:13; 1 Nya 29:29; Isa 30:10; Amo 7:12]

10Basi Sauli akamwambia mtumishi wake, Umesema vema; haya! Twende. Wakaenda mpaka mji ule aliokuwamo mtu wa Mungu.

11Walipokuwa wakikwea mjini, wakakutana na wasichana, waliokuwa wakienda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?[#Mwa 24:11; Kut 2:16]

12Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu watu wana dhabihu leo katika mahali pa juu;[#Mwa 31:54; 1 Sam 16:2; 1 Fal 3:2]

13mkiingia mjini tu, mara mtamwona, kabla hajakwea kwenda mahali pa juu ale chakula; maana, watu hawatakula hadi yeye atakapokuja; kwa sababu yeye ndiye anayeibariki dhabihu; ndipo hao watu walioalikwa hula. Basi, kweeni sasa; maana wakati huu ndio mtakapomwona.

14Nao wakakwea kwenda mjini; nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli akawatokea, kwenda mahali pa juu.

15Basi BWANA alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema,[#1 Sam 15:1; 20:2; Zab 25:14; Mk 11:2-4; Mdo 13:21]

16Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikia.[#1 Sam 10:1; 15:1; 16:3; Kut 2:25; 3:7,9]

17Hata Samweli alipomwona Sauli, BWANA akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia juu zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu.[#1 Sam 16:12; Hos 13:11]

18Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi?

19Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako.

20Na wale punda wako waliopotea siku hizi tatu, usisumbuke kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?

21Basi Sauli akajibu, akasema, Je! Mimi si Mbenyamini, mtu wa kabila iliyo ndogo kuliko kabila zote za Israeli? Na jamaa yangu nayo si ndogo kuliko jamaa zote za kabila la Benyamini? Kwa nini basi, kuniambia hivyo?[#Amu 20:46; Zab 68:27; Amu 6:15]

22Naye Samweli akamtwaa Sauli na mtumishi wake, akawaleta ndani sebuleni, akawaketisha mahali pa heshima kati ya watu walioalikwa, nao jumla yao walikuwa kama watu thelathini.

23Samweli akamwambia mpishi, Lete ile sehemu niliyokupa, hiyo niliyokuambia, Iweke kando.

24Basi mpishi akatwaa paja, na nyama iliyokuwa juu yake, akaiweka mbele ya Sauli. Samweli akasema, Iliyowekwa kando ndiyo hiyo! Iweke mbele yako ule, kwa sababu umewekewa hiyo wewe hadi wakati uliokusudiwa, maana nilisema, Nimewaalika watu. Basi Sauli akala pamoja na Samweli siku hiyo.[#Law 7:32; Eze 24:4; Mdo 10:9; #9:24 maana katika Kiebrania si dhahiri.]

25Hata waliposhuka kutoka mahali pa juu na kufika mjini, akaongea na Sauli darini.[#Kum 22:8]

26Nao wakaamka alfajiri; kisha ikawa, kulipopambazuka, Samweli akamwita Sauli darini, akisema, Amka, nikusindikize urudi kwenu. Basi Sauli akainuka, nao wakatoka wote wawili, yeye na Samweli.

Samweli amtia Sauli mafuta

27Hata walipokuwa wakishuka kuelekea viunga vya mji, Samweli akamwambia Sauli, Mwambie mtumishi atutangulie, naye akitangulia, wewe nawe simama hapa kwa muda, ili nikuambie neno la Mungu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya