1 Timotheo 5

1 Timotheo 5

Huduma kwa waumini

1Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na wanaume vijana kama ndugu;[#Law 19:32]

2wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote.

3Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli.

4Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu.

5Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku.[#Yer 49:11; Lk 2:37; 18:7]

6Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai.

7Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama.

8Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.

9Mjane asiandikwe isipokuwa umri wake amepata miaka sitini; naye amekuwa mke wa mume mmoja;

10na awe ameshuhudiwa kwa matendo mema; katika kulea watoto, kuwa mkaribishaji, kuwaosha watakatifu miguu, kuwasaidia wateswao, na kujitolea kutenda wema katika hali zote.[#Ebr 13:2; Yn 13:14]

11Bali wajane walio vijana ukatae kuwaandika hao, maana, wakizidiwa na tamaa kinyume cha Kristo, wataka kuolewa;

12nao wana hukumu kwa kuwa wameiacha imani yao ya kwanza.

13Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizungukazunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa.[#2 The 3:11]

14Basi napenda wajane, ambao si wazee, waolewe, wazae watoto, watunze nyumba zao; ili wasimpe adui nafasi ya kulaumu.[#1 Kor 7:9]

15Kwa maana wengine wamekwisha kugeuka na kumfuata Shetani.

16Mwanamke aaminiye, akiwa na jamaa walio wajane wa kweli, na awasaidie mwenyewe, kanisa lisilemewe; ili liwasaidie wale walio wajane kweli kweli.

17Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kutoa unabii na kufundisha.[#Rum 12:8; Flp 2:29]

18Kwa maana andiko lasema, Usimfunge kinywa ng'ombe apurapo nafaka. Na tena, Mtenda kazi astahili ujira wake.[#Kum 25:4; 24:15; 1 Kor 9:9; Mt 10:10; Lk 10:7]

19Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.[#Kum 17:6; 19:15; Mt 18:16; 2 Kor 13:1]

20Wale wadumuo kutenda dhambi uwakemee mbele ya wote, ili na wengine waogope.[#Gal 2:14]

21Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, na mbele za malaika wateule, uyatende hayo pasipo kuhukumu kwa haraka; usifanye neno lolote kwa upendeleo.[#Lk 9:26]

22Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi.[#1 Tim 4:14]

23Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo kidogo, kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.

24Dhambi za watu wengine ziko dhahiri, zatangulia kwenda hukumuni; wengine dhambi zao zawafuata.

25Vivyo hivyo matendo yaliyo mazuri yako dhahiri; wala yale yasiyo dhahiri hayawezi kusitirika.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya