2 Mambo ya Nyakati 11

2 Mambo ya Nyakati 11

Yuda na Benyamini wajiimarisha

1Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na Benyamini, watu wateule elfu mia moja na themanini waliokuwa hodari, watu wa vita, ili wapigane juu ya Israeli, ili wamrudishie Rehoboamu huo ufalme.[#1 Fal 12:21]

2Lakini neno la BWANA likamjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema,[#Kum 33:1; 1 Sam 2:27; 1 Fal 12:22-24; 2 Nya 8:14; 12:15; 1 Tim 6:11]

3Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, uwaambie na Israeli wote waliomo Yuda na Benyamini, ukisema,

4BWANA asema hivi, Hamtapanda wala kupigana na ndugu zenu; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi wakayatii maneno ya BWANA wakarudi wasiende kupigana na Yeroboamu.

5Naye Rehoboamu akakaa Yerusalemu, akajenga miji yenye ngome katika Yuda.

6Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa,[#Mwa 35:19; 1 Sam 17:12; Mt 2:1; Amu 15:8; 1 Nya 4:31; 2 Sam 14:2; 2 Nya 20:20; Neh 3:5; Yer 6:1; Amo 1:1]

7Beth-suri, Soko, Adulamu,

8Gathi, Maresha, Zifu,

9Adoraimu, Lakishi, Azeka,

10Sora, Aiyaloni, na Hebroni, iliyoko katika Yuda na Benyamini, miji yenye maboma.

11Akazifanya imara hizo ngome, akaweka majemadari humo, na akiba ya vyakula, na mafuta, na mvinyo.

12Na ndani ya miji yote mmoja mmoja aliweka ngao na mikuki, akaifanya kuwa na nguvu nyingi mno. Yuda na Benyamini ikawa milki yake.

Makuhani na Walawi aamuunga Rehoboamu mkono

13Makuhani na Walawi waliokuwa katika Israeli yote wakamwendea, kutoka maeneo yao yote.

14Walawi wakaacha malisho yao, na milki yao, wakaja Yuda na Yerusalemu; kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwakataza, ili wasimfanyie BWANA ukuhani;[#Hes 35:2; Yos 21:20-42; 1 Fal 12:28-33; 2 Nya 13:9]

15naye akajiwekea makuhani wa mahali pa juu, na wa wale majini, na wa zile ndama alizozitengeneza.[#1 Fal 12:31; 13:33; 14:9; Hos 13:2; Law 17:7; Kum 32:15-17; 1 Kor 10:20; Ufu 16:14; 1 Fal 12:28]

16Na kutoka katika kabila zote za Israeli, wakaandamwa na hao waliojikaza nia kumtafuta BWANA, Mungu wa Israeli, wakaja Yerusalemu, ili wamtolee dhabihu BWANA, Mungu wa baba zao.[#2 Nya 15:9; 30:11; Zab 69:32]

17Hivyo wakaufanya imara kwa miaka mitatu ufalme wa Yuda, na kumtia nguvu Rehoboamu mwana wa Sulemani; kwa maana muda wa miaka mitatu wakaiendea njia ya Daudi na Sulemani.[#2 Nya 12:1; Hos 6:4; Mt 13:18]

Ndoa za Rehoboamu

18Rehoboamu akaoa mke, Mahalathi binti Yerimothi mwana wa Daudi, na wa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese;

19akamzalia wana, Yeushi, na Shemaria, na Zahamu.[#1 Fal 15:2]

20Kisha baada yake akamwoa Maaka, binti Absalomu; na yeye akamzalia Abiya, na Atai, na Ziza, na Shelomithi.

21Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu kuliko wakeze wote na masuria yake; (maana alioa wake kumi na wanane, na masuria sitini, akazaa watoto wa kiume ishirini na wanane na mabinti sitini).

22Rehoboamu akamteua Abiya, mwana wa Maaka, kuwa mkuu, mtawala kati ya nduguze, kwa kuwa aliazimia kumtawaza awe mfalme.[#Kum 21:15-17]

23Akafanya kwa akili, akawatawanya wanawe wote kati ya nchi zote za Yuda na Benyamini, katika kila mji wenye boma; akawapa vyakula tele. Akawatafutia wake wengi.[#Kum 17:17; 1 Fal 11:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya