The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu, Abiya akaanza kutawala juu ya Yuda.[#1 Fal 15:1]
2Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka binti Urieli wa Gibea. Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.[#2 Nya 11:20]
3Abiya akapanga vita akiwa na jeshi la watu hodari wa vita, watu wateule elfu mia nne; naye Yeroboamu akapanga vita juu yake akiwa na watu wateule elfu mia nane, waliokuwa wanaume mashujaa.
4Basi Abiya akasimama juu ya kilima cha Semaraimu, kilichoko milimani mwa Efraimu, akasema, Nisikieni, enyi Yeroboamu na Israeli wote;[#Yos 18:22]
5je! Haikuwapasa kujua ya kwamba BWANA, Mungu wa Israeli, alimpa Daudi ufalme juu ya Israeli milele, yeye na wanawe kwa agano la chumvi?[#Amu 11:21-24; 1 Sam 16:12,13; 2 Sam 7:12-16; Zab 89:20; Lk 1:31-33; Hes 18:19]
6Lakini Yeroboamu mwana wa Nebati, mtumishi wa Sulemani mwana wa Daudi, akainuka, akamfanyia fitina bwana wake.[#1 Fal 11:26; 12:20,27; 2 Nya 10:19]
7Wakamkusanyikia watu mabaradhuli, wasiofaa kitu, waliojitia nguvu juu ya Rehoboamu mwana wa Sulemani, Rehoboamu alipokuwa kijana na wa moyo mwororo, asiweze kuwazuia.[#Amu 9:4; Zab 26:4; Mit 12:11; Mdo 17:5]
8Hata sasa mwajidhania kuwa mtauzuia ufalme wa BWANA mikononi mwa wana wa Daudi; nanyi mmekuwa jamii kubwa, na kwenu mna ndama za dhahabu alizowafanyia Yeroboamu kuwa miungu.[#Hos 8:6]
9Je! Hamkuwafukuza makuhani wa BWANA, wana wa Haruni, na Walawi; mkajifanyia makuhani kama wafanyavyo watu wa nchi nyingine? Hata yeyote ajaye kujifanya wakfu na ndama, na kondoo dume saba, aweza kuwa kuhani wa hiyo isiyo miungu.[#2 Nya 11:14,15; Kut 29:35]
10Lakini sisi, BWANA ndiye Mungu wetu, wala sisi hatukumwacha; tena tunao makuhani wanaomtumikia BWANA, wana wa Haruni, na Walawi, kwa kazi yao;
11nao humtolea BWANA kila asubuhi, na kila jioni, sadaka za kuteketezwa na fukizo la manukato; mikate ya wonyesho pia huiweka kwa taratibu yake juu ya meza takatifu, na kinara cha dhahabu chenye taa zake, kuwaka kila jioni; kwa maana sisi tunayatunza maagizo ya BWANA, Mungu wetu; bali ninyi mmemwacha.[#2 Nya 2:4; Law 24:2-6; Kut 27:20,21]
12Na tazama, Mungu yu pamoja nasi atutangulie, na makuhani wake wenye parapanda, ili wapige sauti ya kuanza vita juu yenu. Enyi wana wa Israeli, msipigane na BWANA, Mungu wa baba zenu; kwani hamtafanikiwa.[#Kum 20:4; Yos 5:14; Zab 20:7; Hes 10:8; Ayu 15:25,26; Mdo 5:39; 9:4,5]
13Lakini Yeroboamu aliwazungushia waviziao kwa nyuma; basi wao wakawa mbele ya Yuda, na wale waviziao nyuma yao.
14Na Yuda walipotazama nyuma, angalia, vita vikawa mbele na nyuma; wakamlilia BWANA, na makuhani wakapiga parapanda.
15Ndipo wakapiga kelele watu wa Yuda; ikawa, watu na Yuda walipopiga kelele, Mungu akampiga Yeroboamu na Israeli wote mbele ya Abiya na Yuda.[#Hes 32:4; 2 Nya 14:12]
16Wana wa Israeli wakakimbia mbele ya Yuda; naye Mungu akawaua mikononi mwao.
17Abiya na watu wake wakawapiga mapigo makuu; hata wakaanguka wameuawa wa Israeli elfu mia tano, watu wateule.
18Ndivyo walivyotiishwa wana wa Israeli wakati ule, wakashinda wana wa Yuda, kwa kuwa walimtegemea BWANA, Mungu wa baba zao.[#Amu 8:28; 2 Fal 18:5; 1 Nya 5:20; 2 Nya 16:8,9; 20:20; Zab 22:5]
19Abiya akamfuata Yeroboamu, akamnyang'anya miji, Betheli na vijiji vyake na Yeshana na vijiji vyake, na Efroni na vijiji vyake.[#Yos 15:9; Yn 11:54]
20Wala Yeroboamu hakupata nguvu tena siku za Abiya; kisha BWANA akampiga, akafa.[#1 Sam 25:38; 26:10; Eze 24:16; Mdo 12:23; 1 Fal 14:20]
21Ila Abiya akapata nguvu, akaoa wake kumi na wanne, akazaa watoto wa kiume ishirini na wawili, na mabinti kumi na sita.
22Na mambo ya Abiya yaliyosalia, na njia zake, na maneno yake, yameandikwa katika kitabu cha maelezo cha nabii Ido.[#2 Nya 9:29; 12:15]