2 Mambo ya Nyakati 15

2 Mambo ya Nyakati 15

1Ndipo Roho ya Mungu ikamjia Azaria mwana wa Odedi;[#Hes 24:2; Amu 3:10; 2 Sam 23:2; 2 Nya 20:14; 24:20; 2 Pet 1:21]

2naye akatoka ili amlaki Asa, akamwambia, Nisikieni, Ee Asa, na Yuda wote na Benyamini; BWANA yu pamoja nanyi, mkiwa pamoja naye; nanyi mkimtafuta ataonekana kwenu; lakini mkimwacha atawaacha ninyi.[#Yak 4:8; 1 Nya 28:9; 2 Nya 33:12,13; Yer 29:13; Mt 7:7; 2 Nya 12:1-3; 24:20; Rum 11:1,2; Ebr 12:25]

3Basi kwa siku nyingi Israeli wamekuwa hawana Mungu wa kweli, wala hawana kuhani afundishaye, wala hawana torati;[#Hos 3:4; Law 10:11]

4lakini walipomgeukia BWANA, Mungu wa Israeli, katika msiba wao, na kumtafuta, akaonekana kwao.[#Kum 4:29]

5Hata na zamani zile hakukuwa na amani kwake atokaye, wala kwake aingiaye, ila fadhaa kubwa juu yao wote wakaao katika nchi.[#Amu 5:6]

6Walivunjikavunjika, taifa juu ya taifa, na mji juu ya mji; kwa sababu Mungu aliwafadhaisha kwa shida zote.[#Mt 24:7]

7Nanyi jipeni nguvu, wala mikono yenu isilegee; kwa maana kazi yenu itakuwa na thawabu.[#Mwa 15:1; Rut 2:12; Zab 58:11; Mt 5:12-46; Lk 6:35; Kol 3:24]

8Naye Asa alipoyasikia maneno hayo, yaani, unabii wa mwana wa Odedi nabii, akatiwa nguvu, akayaondolea mbali machukizo yote katika nchi ya Yuda na Benyamini, na katika miji aliyoitwaa milimani mwa Efraimu; akaitengeneza upya madhabahu ya BWANA, iliyokuwako mbele ya ukumbi wa BWANA.[#2 Nya 13:19]

9Akakusanya Yuda wote na Benyamini, na hao wageni waliokaa kwao, wa Efraimu, na wa Manase, na wa Simeoni; kwa kuwa walimjia wengi katika Israeli, walipoona kwamba BWANA, Mungu wake, alikuwa pamoja naye.[#2 Nya 11:16]

10Basi wakakusanyika huko Yerusalemu mwezi wa tatu, katika mwaka wa kumi na tano wa kumiliki kwake Asa.

11Wakamchinjia BWANA siku ile, katika nyara walizozileta, dhabihu za ng'ombe mia saba, na kondoo elfu saba.[#2 Nya 14:15]

12Wakafanya agano, ya kuwa watamtafuta BWANA, Mungu wa baba zao, kwa mioyo yao yote, na kwa roho zao zote;[#2 Fal 23:3; 2 Nya 34:31; Neh 10:29]

13na ya kwamba yeyote asiyemtafuta BWANA, Mungu wa Israeli, atauawa, akiwa mdogo au mkubwa, awe ni mwanamume au mwanamke.[#Kut 22:20; Kum 13:5,9,15]

14Wakamwapia BWANA kwa sauti kuu, na kwa kelele, na kwa parapanda, na kwa baragumu.

15Na Yuda wote wakakifurahia kile kiapo; kwani wameapa kwa moyo wao wote, na kumtafuta kwa mapenzi yao pia; naye ameonekana kwao; naye BWANA akawastarehesha pande zote.

16Hata na Maaka mamaye Asa, mfalme akamwondolea cheo chake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake, akaiponda, akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.[#1 Fal 15:2,10]

17Lakini mahali pa juu hapakuondolewa katika Israeli; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu siku zake zote.[#Kum 12:7; 1 Fal 3:2-4; 15:14; 2 Fal 12:3; 2 Nya 14:3,5]

18Akavileta nyumbani mwa Mungu vitu alivyovitakasa babaye, na vile alivyovitakasa mwenyewe, fedha, na dhahabu, na vyombo.

19Wala hapakuwa na vita tena hata mwaka wa thelathini na tano wa kutawala kwake Asa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya