2 Mambo ya Nyakati 17

2 Mambo ya Nyakati 17

Utawala wa Yehoshafati

1Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake, akajitia nguvu juu ya Israeli.

2Akaweka jeshi katika miji yote yenye maboma ya Yuda, akatia na askari walinzi katika nchi ya Yuda, na katika miji ya Efraimu, aliyoitwaa Asa babaye.[#2 Nya 11:11; 15:8]

3Naye BWANA alikuwa pamoja na Yehoshafati, kwa kuwa alikwenda katika njia za kwanza za Daudi babaye, asiyatafute Mabaali;[#Rum 8:31]

4lakini alimtafuta Mungu wa baba yake, akaenda katika amri zake, wala si katika matendo ya Israeli.[#Lk 1:6; 1 Fal 12:28]

5Kwa hiyo BWANA akauthibitisha ufalme mkononi mwake; Yehoshafati akaletewa zawadi na watu wote wa Yuda; basi akawa na mali na heshima tele.[#1 Sam 10:27; 1 Fal 10:25,27; 2 Nya 18:1]

6Ukainuliwa moyo wake katika njia za BWANA; na zaidi ya hayo akapaondoa mahali pa juu, na Maashera, katika Yuda.[#1 Fal 22:43; 2 Nya 14:3; 15:17; 19:3]

7Tena, katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake, akawatuma wakuu wake, yaani, Ben-haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli, na Mikaya, ili kufundisha mijini mwa Yuda;[#2 Nya 15:3]

8na pamoja nao Walawi, yaani, Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adonia, Tobia, na Tob-adonia, Walawi; na pamoja nao Elishama na Yehoramu, makuhani.

9Wakafundisha katika Yuda, wenye kitabu cha Torati ya BWANA; wakazunguka katika miji yote ya Yuda, wakafundisha kati ya watu.[#2 Nya 35:3; Law 10:11; Neh 8:7; Mal 2:7]

10Hofu ya BWANA ikaziangukia falme za nchi zote zilizozunguka Yuda, wasipigane vita na Yehoshafati.[#Mwa 35:5; Kut 15:15; Kum 11:25; 2 Nya 14:14]

11Na baadhi ya Wafilisti walimletea Yehoshafati zawadi, na fedha ya kodi; Waarabu nao wakamletea kondoo dume elfu saba na mia saba, na mabeberu elfu saba na mia saba.[#2 Sam 8:2]

12Ukuu wake Yehoshafati ukazidi sana; akajenga katika Yuda ngome na miji ya hazina.

13Naye alikuwa na kazi nyingi katika miji ya Yuda; na watu wa vita, watu mashujaa humo Yerusalemu.

14Na hivi ndivyo walivyohesabiwa kwa mbari za baba zao; wa Yuda, makamanda wa maelfu; Adna jemadari, na pamoja naye watu mashujaa elfu mia tatu;

15na wa pili wake Yehohanani kamanda, na pamoja naye elfu mia mbili na themanini;

16na baada yake Amasia mwana wa Zikri, aliyejitoa kwa BWANA kwa moyo, na pamoja naye elfu mia mbili, watu mashujaa;[#Amu 5:2,9; 1 Nya 29:9-17; Zab 110:3; 2 Kor 8:12]

17na wa Benyamini; Eliada mtu shujaa, na pamoja naye elfu mia mbili wenye nyuta na ngao;

18na wa pili wake Yehozabadi, na pamoja naye elfu mia moja na themanini waliojiweka tayari kwa vita.

19Hao ndio waliomngojea mfalme, zaidi ya hao mfalme aliowaweka katika miji yenye maboma katika Yuda yote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya