The chat will start when you send the first message.
1Yehoshafati mfalme wa Yuda akarudi Yerusalemu nyumbani kwake kwa amani.
2Yehu mwana wa Hanani mwonaji akatoka kwenda kumlaki, akamwambia mfalme Yehoshafati, Je! Imekupasa kuwasaidia waovu, na kuwapenda wamchukiao BWANA? Kwa ajili ya hayo ghadhabu itokayo kwa BWANA i juu yako.[#1 Sam 9:9; Zab 15:4; Mit 1:10; 2 Nya 32:25]
3Walakini, yameonekana kiasi cha mema ndani yako, kwa kuwa umeyaondoa Maashera katika nchi, na moyo wako umeukaza kumtafuta Mungu.[#2 Nya 12:12; 30:19; Ezr 7:10]
4Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa BWANA, Mungu wa baba zao.
5Akateua waamuzi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji;[#Kum 16:18]
6akawaambia hao waamuzi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila BWANA; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu.[#Kum 1:17; Zab 82:1; Mhu 5:8]
7Basi sasa hofu ya BWANA na iwe juu yenu; aiweni waangalifu katika jambo mtendalo, kwa maana kwa BWANA, Mungu wetu hakuna upotoshaji wala kupendelea nafsi za watu au kupokea rushwa.[#Kum 32:4; Rum 9:14; Kum 10:17; Ayu 34:19; Mdo 10:34; Rum 2:11; Gal 2:6; Efe 6:9; Kol 3:25; 1 Pet 1:17]
8Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akateua baadhi ya Walawi na makuhani, na wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi kwa hukumu za BWANA na kesi kati yao. Nao wakarudi Yerusalemu.[#Kum 16:18; 17:9-13; 1 Nya 23:4; 26:19; 2 Nya 17:8]
9Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya BWANA, kwa uaminifu, na kwa moyo wote.[#2 Sam 23:3]
10Na kila mara watakapowaletea shitaka toka ndugu zenu wakaao mijini mwao, kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria na amri, kanuni au maagizo, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za BWANA, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.[#Kum 17:8; Hes 16:46; Eze 3:18]
11Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yuko juu yenu kwa maneno yote ya BWANA; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa mambo yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye BWANA awe pamoja nao walio wema.