2 Mambo ya Nyakati 22

2 Mambo ya Nyakati 22

Utawala wa Ahazia

1Nao wakazi wa Yerusalemu walimfanya Ahazia mwanawe mdogo awe mfalme mahali pake; maana wakubwa wake wote wamekwisha kuuawa na kikosi cha watu waliokuja kambini pamoja na Waarabu. Hivyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akatawala.[#2 Fal 8:24; 2 Nya 21:17]

2Ahazia alikuwa na umri wa miaka arubaini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri.[#2 Fal 8:26; 1 Fal 16:28; 2 Nya 21:6]

3Yeye naye akazifuata njia za nyumba ya Ahabu; kwa kuwa mamaye alikuwa mshauri wake katika kufanya maovu.

4Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kama nyumba ya Ahabu; kwa kuwa hao walikuwa washauri wake, baada ya kifo cha baba yake, hata aangamie.[#2 Nya 24:17,18; Mit 1:10; 19:27]

5Naye akaenda kwa mashauri yao, akafuatana na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamjeruhi Yoramu.[#2 Fal 8:28; #22:5 Au, Yehoramu.]

6Akarudi Yezreeli ili aponye majeraha waliyomjeruhi huko Rama, alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu, katika Yezreeli, kwa sababu alikuwa mgonjwa.[#2 Fal 9:15; #22:6 Au, Azaria.]

7Basi kuangamia kwake Ahazia kulitokana na Mungu, kwa vile alivyomwendea Yoramu; kwa kuwa alipofika, akatoka pamoja na Yoramu juu ya Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alimtia mafuta ili awakatilie mbali nyumba ya Ahabu.[#Amu 14:4; 1 Fal 12:15; 2 Nya 10:15; Zab 5:10; 9:16; Amo 3:6; Mdo 2:23; 1 Fal 19:16; 2 Fal 9:6,7,21]

8Ikawa, Yehu alipokuwa akiwafanyia hukumu nyumba ya Ahabu, aliwakuta wakuu wa Yuda, na wana wa nduguze Ahazia, wakimtumikia Ahazia, akawaua.[#2 Fal 10:10,11]

9Akamtafuta Ahazia, wakamkamata, (naye alikuwa amejificha Samaria,) wakamleta kwa Yehu, wakamwua; wakamzika, kwa maana wakasema, Huyu ni mwana wa Yehoshafati, huyo aliyemtafuta BWANA kwa moyo wake wote. Wala nyumba ya Ahazia hawakuwa na uwezo wa kuushika ufalme.[#2 Fal 9:27]

Athalia akivamia kiti cha ufalme

10Basi Athalia, mama wa Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaangamiza jamaa yote ya kifalme ya nyumba ya Yuda.

11Ila Yehosheba, binti mfalme, akamtwaa Yoashi, mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa, akamweka yeye na yaya wake katika chumba cha kulala. Basi Yehosheba, binti mfalme Yehoramu, mkewe Yehoyada kuhani, (naye alikuwa dada yake Ahazia,) akamficha ili Athalia, asimwue.[#2 Fal 11:2]

12Akawako pamoja nao, amefichwa nyumbani mwa Mungu, miaka sita. Na Athalia akaitawala nchi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya