2 Mambo ya Nyakati 30

2 Mambo ya Nyakati 30

Pasaka Kuu

1Hezekia akatuma wajumbe kwa Israeli wote na Yuda pia; akawaandikia nyaraka Efraimu na Manase, waje nyumbani kwa BWANA Yerusalemu, ili wamfanyie Pasaka BWANA, Mungu wa Israeli.

2Kwa maana mfalme na wakuu wake, na kusanyiko lote katika Yerusalemu walikubaliana kuiadhimisha Pasaka mwezi wa pili.[#Hes 9:10]

3Kwa sababu hawakuweza kuifanya wakati ule, kwa kuwa makuhani wa kutosha walikuwa hawajajitakasa, wala watu hawajakusanyika huko Yerusalemu.[#Kut 12:6; 2 Nya 29:34]

4Likawa neno jema machoni pa mfalme, na kusanyiko lote.

5Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie Pasaka BWANA, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.

6Matarishi, kwa amri ya mfalme na maofisa wake wakapeleka nyaraka katika Israeli na Yuda yote, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni BWANA, Mungu wa Abrahamu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia ninyi mlionusurika na kuokoka toka mikononi mwa Wafalme wa Ashuru.[#1 Sam 7:3,4; Isa 55:6,7; Hos 6:1; 14:1; Yoe 2:13; Mal 3:7; 2 Fal 15:19,29]

7Wala msiwe kama baba zenu, na kama ndugu zenu, waliomwasi BWANA, Mungu wa baba zao, hata akawatoa kuwa ukiwa, kama mwonavyo.[#Eze 20:18; 2 Nya 29:8]

8Msiwe sasa wenye shingo ngumu kama baba zenu; lakini mjitoe kwa BWANA, mkaingie katika patakatifu pake, alipopatakasa milele, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu, hasira yake kali iwageukie mbali.[#Kum 10:16; 2 Nya 29:10]

9Kwa kuwa mkimrudia BWANA, ndugu zenu na watoto wenu watahurumiwa machoni pa hao waliowachukua mateka, nao watairudia nchi hii; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye mwenye neema, na mwenye rehema, wala hatawageuzia mbali uso wake, mkimrudia.[#Law 26:40; Kut 34:6; Zab 86:5,15; Mik 7:18; Isa 55:7]

10Basi matarishi wakapita mji kwa mji kati ya nchi ya Efraimu na Manase, hata kufika Zabuloni; lakini waliwacheka na kuwadhihaki.[#2 Nya 36:16; Neh 2:19; Yer 5:12; Mt 21:35; Lk 8:53; Mdo 17:32; Ebr 11:36]

11Ila watu wengine wa Asheri, na wa Manase, na wa Zabuloni walijinyenyekeza, wakaja Yerusalemu.[#2 Nya 11:16]

12Tena katika Yuda mkono wa Mungu ulikuwa ukiwapa moyo mmoja, waitimize amri ya mfalme na wakuu kwa neno la BWANA.[#2 Nya 29:25,36; Ezr 7:27; Zab 110:3; 2 Kor 3:5; Flp 2:13; Ebr 13:21]

13Basi watu wengi wakakusanyika Yerusalemu watu wengi ili kuifanya sikukuu ya mikate isiyochachwa katika mwezi wa pili, kusanyiko kuu sana.

14Wakainuka, wakaziondoa madhabahu zilizokuwamo Yerusalemu, nazo madhabahu za kufukizia wakaziondoa, wakazitupa katika kijito Kidroni.[#2 Nya 28:24; Isa 2:17-21]

15Kisha wakaichinja Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa pili, nao makuhani na Walawi wakatahayarika, wakajitakasa, wakaleta sadaka za kuteketezwa nyumbani mwa BWANA.[#2 Nya 29:34]

16Wakasimama mahali pao kwa taratibu yao, kulingana na Torati ya Musa, mtu wa Mungu; nao makuhani wakainyunyiza damu, waliyoipokea mikononi mwa Walawi.

17Kwa maana kulikuwa na wengi katika kusanyiko ambao hawajajitakasa; kwa hiyo Walawi wakamchinjia Pasaka, kila mtu asiyekuwa safi, ili kuwatakasa kwa BWANA.[#2 Nya 29:34]

18Kwani wingi wa watu, naam, wengi wa Efraimu, na wa Manase, na wa Isakari, na wa Zabuloni, hawakujisafisha, lakini wakala Pasaka, ila si kama ilivyoandikwa. Naye Hezekia alikuwa amewaombea, akisema, BWANA mwema na amsamehe kila mtu,[#Kut 12:43]

19aukazaye moyo wake kumtafuta Mungu, BWANA, Mungu wa babaze, hata ikiwa si kwa utakaso wa patakatifu.[#1 Sam 7:3; 1 Nya 29:18; 2 Nya 19:3; 20:33; Ezr 7:10; Ayu 11:13]

20BWANA akamsikia Hezekia, akawaponya watu.[#Kut 15:26; Zab 103:3; Yak 5:16]

21Nao wana wa Israeli waliokusanyika Yerusalemu wakafanya sikukuu ya mikate isiyochachwa siku saba kwa furaha kubwa; Walawi na makuhani wakamsifu BWANA siku kwa siku, wakimwimbia BWANA kwa vinanda vyenye sauti kuu.[#Kut 12:15; 13:6; Law 23:6; Lk 22:1-7; 1 Kor 5:7,8]

22Hezekia akawafurahisha mioyo Walawi wote waliokuwa mastadi wa kumtumikia BWANA. Basi muda wa siku saba wakala sikukuu, wakitoa dhabihu za sadaka za amani, na kumtolea shukrani BWANA, Mungu wa baba zao.[#Isa 40:2; Kum 33:10; 2 Nya 17:9; 35:3; 2 Tim 4:2; Ezr 10:11]

23Na kusanyiko lote wakafanya shauri kufanya sikukuu siku saba nyingine; wakafanya sikukuu siku saba nyingine kwa furaha.[#1 Fal 8:65]

24Maana Hezekia, mfalme wa Yuda, aliwatolea kusanyiko matoleo ya ng'ombe elfu moja, na kondoo elfu saba; na wakuu wakawatolea kusanyiko ng'ombe elfu moja, na kondoo elfu kumi; tena wakajitakasa makuhani wengi sana.[#2 Nya 35:7,8; 29:34]

25Na kusanyiko lote la Yuda, pamoja na makuhani na Walawi, na kusanyiko lote waliotoka Israeli, na wageni waliotoka katika nchi ya Israeli, nao waliokaa Yuda, wakafurahi.[#2 Nya 30:11,18]

26Ikawa furaha kuu katika Yerusalemu; kwa sababu tangu siku za Sulemani mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli, hayajakuwako mambo kama hayo huko Yerusalemu.

27Ndipo wakasimama makuhani Walawi, wakawabariki watu; ikasikiwa sauti yao, sala yao ikafika hata makao yake matakatifu, yaani, mbinguni.[#Hes 6:23; Zab 68:5; Isa 57:15; 66:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya