The chat will start when you send the first message.
1Lakini nafsini mwangu nilikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni.[#2 Kor 12:21; 1 Kor 4:21]
2Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami?
3Nami niliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia.
4Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia nikiwa na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi.[#Mdo 20:31]
5Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote.[#1 Kor 5:1]
6Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi;
7hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi.
8Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu.
9Maana niliandika kwa sababu hii pia, ili nipate wazi kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote.[#2 Kor 7:15]
10Lakini kama mkimsamehe mtu neno lolote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lolote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo,[#Lk 10:16]
11Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.[#Lk 22:31]
12Basi nilipofika Troa kwa ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana,[#Mdo 20:1; 14:27; 1 Kor 16:9]
13sikuona raha nafsini mwangu, kwa sababu sikumwona Tito ndugu yangu, bali niliagana nao, nikaondoka kwenda Makedonia.
14Ila Mungu ashukuriwe, anayetufanya tushangilie ushindi daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu.
15Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea;[#1 Kor 1:18]
16katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?[#2 Kor 3:5,6; Lk 2:34]
17Kwa maana sisi si kama walio wengi, walichuuzao neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo.[#2 Kor 1:12; 1 Pet 4:11]