The chat will start when you send the first message.
1Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.[#2 Kor 1:24; 5:20]
2(Kwa maana asema,[#Isa 49:8; Lk 4:19,21]
Kwa wakati uliokubalika nilikusikia,
Na katika siku ya wokovu nilikusaidia;
tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.)
3Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe;
4bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika subira nyingi, katika mateso, katika shida, katika matatizo;[#2 Kor 4:2]
5katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga;[#Mdo 16:23; 2 Kor 11:23-27]
6katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki;[#1 Tim 4:12]
7katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kulia na za mkono wa kushoto;[#1 Kor 2:4]
8kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli;
9kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa;[#2 Kor 4:10; Zab 118:18]
10kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.[#Flp 4:12,13]
11Vinywa vyetu vimefumbuliwa kwenu, enyi Wakorintho; mioyo yetu imekunjuliwa.[#Zab 119:32]
12Hamsongwi ndani yetu, bali mwasongwa katika mioyo yenu.
13Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa (nasema nanyi kama na watoto), nanyi pia mkunjuliwe mioyo.[#1 Kor 4:14]
14Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?[#Efe 5:11]
15Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?[#6:15 maana yake ni, Ufisadi.]
16Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.[#Law 26:12; Eze 37:27; 1 Kor 3:16; 6:19; Eze 37:27]
17Kwa hiyo,[#Isa 52:11; Yer 51:45; Eze 20:34,41; Ufu 18:4]
Tokeni kati yao,
Mkatengwe nao, asema Bwana,
Msiguse kitu kilicho kichafu,
Nami nitawakaribisha.
18Nitakuwa Baba kwenu,[#2 Sam 7:8,14; 1 Nya 17:13; Isa 43:6; Yer 31:9; 32:38; Hos 1:10; Amo 4:13]
Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,
asema Bwana Mwenyezi.