2 Wafalme 18

2 Wafalme 18

Hezekia atawala Yuda

1Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.[#2 Nya 28:27; 29:1]

2Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na tisa katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.[#2 Nya 29:1]

3Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.

4Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani.[#2 Nya 31:1; Hes 21:9; #18:4 maana yake ni ‘kipande cha shaba.’]

5Alimtumaini BWANA, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.[#2 Fal 19:10; 2 Nya 32:7,8; Ayu 13:5; 27:1,2; Mt 27:43; Efe 1:12; 2 Fal 23:25]

6Maana alishikamana na BWANA, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake BWANA alizomwamuru Musa.[#Kum 10:20; Yos 23:8]

7Naye BWANA akawa pamoja naye, kila alikokwenda alifanikiwa; tena alimwasi mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.[#Mwa 39:2,3; 2 Nya 15:2; Zab 46:11; 60:12; Mt 1:23; 1 Sam 18:5; 2 Fal 16:7]

8Akawapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake, tangu mnara wa walinzi hata mji wenye boma.[#1 Nya 4:41; Isa 14:29]

9Hata katika mwaka wa nne wa Hezekia, ndio mwaka wa saba wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, akakwea ili kupigana na Samaria, akauhusuru.[#2 Fal 17:3]

10Wakautwaa baada ya miaka mitatu; yaani, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ndio mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Israeli, ndipo Samaria ulipotwaliwa.[#2 Fal 17:6]

11Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi;[#1 Nya 5:26]

12kwa sababu hawakuitii sauti ya BWANA, Mungu wao, bali waliyavunja maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.[#2 Fal 17:7; 1 Fal 9:6; Dan 9:6,10]

Senakeribu avamia Yuda

13Ikawa katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.[#2 Nya 32:1; Isa 36:1]

14Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; chochote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini.

15Hezekia akampa fedha yote iliyoonekana katika nyumba ya BWANA, na katika hazina za nyumba ya mfalme.[#1 Fal 15:15-19; 2 Fal 12:18; 16:8; 2 Nya 12:9; 28:21]

16Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la BWANA, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru.

17Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na kamanda wake, toka Lakishi, kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika, wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea Uwanda wa Dobi.[#Isa 7:3; #18:17 Au, akawatuma Tartani, na Rabsarisi, na Rabshake.]

18Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.

19Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kusema, Mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?[#2 Nya 32:10; #18:19 Au, Rabshake.]

20Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?[#Ezr 4:15]

21Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.[#Isa 36:6; Eze 29:6,7]

22Lakini mkiniambia, Tunamtumaini BWANA, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu?[#2 Nya 31:1; 32:12; Isa 36:7]

23Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.

24Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa ofisa mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?

25Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la BWANA? BWANA ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.[#1 Fal 13:18; 2 Fal 19:6,22; 2 Nya 35:21; Isa 7:17; 10:5,19]

26Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule kamanda, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa hao watu walio ukutani.

27Lakini yule kamanda akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Je! Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?

28Kisha yule kamanda akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.

29Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake.[#2 Nya 32:15; Ayu 5:19; Dan 3:15,17; 6:16]

30Wala Hezekia asiwatumainishe katika BWANA, akisema, Hakika BWANA atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.

31Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe;[#Mwa 32:20; 33:11; Mit 18:16]

32hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, BWANA atatuokoa.[#Kum 8:7,8]

33Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wowote na mkono wa mfalme wa Ashuru?[#2 Fal 19:12; 2 Nya 32:14; Isa 10:10,11]

34Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu?[#2 Fal 19:13; Yer 49:23; 2 Fal 17:24]

35Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata BWANA auokoe Yerusalemu na mkono wangu?[#Zab 2:2,4; 50:21; Isa 10:5-15; 42:8; Dan 3:15; Rum 1:21-23]

36Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno.

37Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule kamanda.[#Ayu 1:20; Isa 33:7; 36:21,22; Yer 36:24]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya