The chat will start when you send the first message.
1Ikatokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe.[#Ebr 11:35-36]
2Mmoja akajifanya mnenaji wao, akasema, Wataka kuuliza nini na kujua nini juu yetu? Sisi tu tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu.
3Mfalme akaghadhibika sana, akaamuru yapashwe moto masufuria na makaango;
4nayo yalipokolea alitoa amri ya kumkata ulimi yule aliyekuwa mnenaji wao, na kumchuna ngozi ya kichwa, na kuikatilia mbali mikono yake na miguu yake, machoni pa ndugu zake na mama yake.
5Hata, alipobaki kiwiliwili tu, aliagizwa aletwe motoni, angali yu hai, akaangwe katika kaango. Moshi wa kaangoni ulipoenea, watoto na mama yao walitiana moyo wafe kwa ushujaa,
6wakisema, BWANA Mungu anatuangalia, naye kweli atatuonesha rehema, kama Musa alivyosema katika wimbo wake, unaowashuhudia waziwazi: Atawahurumia watumwa wake.[#Kum 32:36]
7Wa kwanza alipokufa hivyo, walimleta wa pili adhihakiwe. Wakamchuna ngozi ya kichwa pamoja na nywele zake, wakamwuliza, Je, utakula, kabla ya kuteswa viungo vyote vya mwili wako?
8Akajibu kwa lugha ya wazee wake, akawaambia, La! Basi, yeye pia aliteswa yale mateso yote kwa mfululizo, kama yule wa kwanza.
9Naye alipokuwa kufani alisema, Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele.
10Na baada yake alidhihakiwa yule wa tatu. Naye mara alipoagizwa, alitoa ulimi wake, akanyosha mikono yake bila hofu,
11akasema kwa ushujaa, Kutoka mbinguni nilipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena.
12Hata mfalme na watu wake walishangazwa kwa roho ya kijana huyu, kwa jinsi alivyoyadharau maumivu yake.
13Akiisha kufa huyu, walimtesa wa nne na kumtendea mabaya yale yale.
14Naye alipokaribia kufa alisema hivi: Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo.
15Baada yake wakamchukua wa tano na kumtenda vibaya mno.
16Naye akamtazama mfalme akasema, Wewe, ingawa u kiumbe tu, una mamlaka juu ya watu; kwa hiyo watenda upendavyo. Lakini usifikiri ya kuwa taifa letu limetupwa na Mungu.
17Endelea tu, nawe utauona uweza wake mkuu, jinsi atakavyokutesa wewe na uzao wako.
18Na baada yake walimchukua wa sita. Naye alipokaribia kufa alisema, Usidanganyike bure. Sisi tunateswa hivi kwa sababu ya dhambi zetu wenyewe, kwa kuwa sisi tumemkosa Mungu wetu. Ndiyo sababu mambo haya ya kutisha yametupata.
19Lakini usifikiri utaepukana na adhabu, wewe uliyejaribu kupigana na Mungu.
20Lakini aliyekuwa wa ajabu hasa, na kustahili kumbukumbu la heshima, ndiye yule mama. Maana aliwaona wanawe saba wakifa kwa siku moja, akistahimili kwa moyo thabiti kwa ajili ya matumaini aliyoyaweka kwa BWANA.
21Kwa roho hodari aliimarisha tabia yake ya kike kwa ushupavu wa kiume, akamfariji kila mtoto kwa lugha ya wazee wao,
22akisema, Jinsi mlivyoingia tumboni mwangu sijui. Si mimi niliyekupeni roho na uzima, wala si mimi niliyeziunga sehemu za miili yenu.
23Bali ni yeye, Muumba ulimwengu; yeye ambaye wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa rehema zake atakurudishieni roho zenu na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa mnajihesabu kuwa si kitu kwa ajili ya amri zake.
24Antioko alijiona anafedheheshwa, lakini bila kuangalia mzaha wa maneno yake, alimsihi yule mdogo, maana alikuwa yungali hai, akamwambia, si kwa maneno tu ila pia kwa kuapa, ya kuwa, kama ataziacha sheria za wazee wake, atampatia mali nyingi na hali njema; tena atamfanya mmoja wa rafiki zake na kumkabidhi kazi za ufalme.
25Yule kijana asipokubali, alimwita mama yake, akamtaka amshawishi mtoto ajiokoe.
26Akasema naye kwa maneno mengi, hata mwisho alikubali kumshauri mwanawe.
27Akamwinamia – na huku anamdhihaki yule mfalme mkali – akasema hivi kwa lugha ya wazee wake: Mwanangu, unirehemu mimi niliyekuchukua tumboni mwangu kwa miezi tisa, na kukunyonyesha kwa miaka mitatu, na kukutunza na kukulea mpaka sasa.
28Nakusihi, mwanangu, inua macho yako utazame mbingu na nchi, ukaone vitu vyote vilivyomo; fahamu kwamba Mungu hakuviumba kwa vitu vilivyokuwapo. Na ndivyo alivyofanya wanadamu pia.
29Usimwogope mwuaji huyu; jioneshe umestahimili sawasawa na ndugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu nikupokee tena pamoja na ndugu zako.
30Hakudiriki kuyamaliza maneno yake, ila yule kijana alisema, Mnamngoja nani? Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa Musa.
31Wewe, uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania, hutaokoka kabisa katika mikono ya Mungu.
32Sisi tunateswa kwa ajili ya dhambi zetu wenyewe;
33na kama Mungu wetu aliye hai anatuonya na kutuadhibu katika hasira yake ya kitambo, atapatanishwa tena na wale walio watumsihi wake mwenyewe.
34Ila wewe, mtu mbaya, mwovu kuliko wote, usijivune katika jeuri yako na tumaini lako la bure, na kuinua mkono wako juu ya wana wa mbinguni, maana hujaepukana na hukumu ya Mwenyezi Mungu aonaye yote.
35Hawa ndugu zetu waliovumilia waumivu mafupi
36wamekunywa sasa chemchemi ya uzima wa milele katika agano la Mungu. Bali wewe, katika hukumu ya Mungu, utapokea kwa kipimo cha haki adhabu za jeuri yako.
37Mimi, kama ndugu zangu, natoa mwili wangu na roho yangu kwa ajili ya amri za baba zetu, nikimsihi Mungu alifadhili taifa letu upesi, na kwa mateso na mapigo akulazimishe wewe kukiri kwamba yeye ndiye Mungu peke yake;
38na katika mimi na ndugu zangu hasira ya Mungu ikomeshwe, ambayo kwa haki imelishika taifa letu lote.
39Mfalme akakasirika mno, na kuona uchungu kwa jinsi alivyodhihakiwa kwa hiyo alimtesa huyu vibaya kuliko wale wengine.
40Naye pia alikufa yu safi, akimtumaini BWANA kwa moyo wake wote.
41Na baada ya wanawe wote alikufa huyu mama.
42Hayo yatosha juu ya dhabihu na ukatili wa kishenzi wa mfalme.