2 Wathesalonike 2

2 Wathesalonike 2

Mtu wa uvunjaji sheria

1Basi, ndugu, tunawasihini, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake,[#1 The 4:15-17]

2kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msishtushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa barua inayodhaniwa kuwa ni yetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

3Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yoyote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu;[#1 Tim 4:1; Yn 17:12; 1 Yoh 2:18; 4:3]

4yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama cha kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.[#Dan 11:36; Eze 28:2]

5Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi niliwaambia hayo?

6Na sasa lizuialo mnalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inafanya kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hadi atakapoondolewa.[#Mdo 20:29]

8Hapo ndipo atakapofunuliwa yule mwasi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa dhihirisho la kuja kwake;[#Isa 11:4; Ayu 4:9; Ufu 19:15,20]

9kuja kwa yule mwasi ni kazi ya Shetani, atumiaye uwezo wote, ishara na ajabu za uongo;[#Mt 24:24; Ufu 13:11-13]

10na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.[#2 Kor 2:15; 4:3]

11Kwa hiyo Mungu anawaletea upotevu mwingi, wauamini uongo;[#2 Tim 4:4]

12ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.

Waliochaguliwa kwa wokovu

13Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli;[#Efe 1:4; Kum 33:12; 1 The 2:13; 4:7]

14aliyowaitia ninyi kwa Injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.[#1 The 4:7; 5:9]

15Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa barua yetu.

16Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema,[#1 The 3:11-13]

17awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya