Kumbukumbu la Torati 6

Kumbukumbu la Torati 6

Amri kuu

1Na hii ndiyo sheria, amri na hukumu, alizoziamuru BWANA, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayovuka kuimiliki;

2upate kumcha BWANA, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe.[#Kut 20:2-20; Zab 111:10; 128:1; Mhu 12:13; Mit 3:1]

3Sikiliza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama BWANA, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali.

4Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja[#Mk 12:29; Isa 9:6; Yn 1:1; 10:30; 17:3; 1 Kor 8:4; Efe 4:6; Flp 2:5,6; #6:4 Au Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; au Bwana Mungu wetu ni mmoja; au Bwana ni Mungu wetu, Bwana ni mmoja.]

5Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.[#Mt 22:37; Mk 12:30-32; Lk 10:27; Kum 30:6; 1 Yoh 5:3]

6Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako;[#Kum 11:18-20; Isa 51:7]

7nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyasema uishipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.[#Efe 6:4]

8Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako.[#Mit 6:21; Kut 13:9; Mit 3:3; 7:3]

9Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.[#Kum 11:20; Isa 50:8; 57:8]

Hadhari ya kutotii

10Kisha BWANA Mungu wako atakapokuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Abrahamu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe,[#Mwa 12:7; 26:3; 28:13; Yos 24:13; Zab 105:44]

11na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vilivyochimbwa usivyochimba wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba;

12ndipo ujitunze, usije ukamsahau BWANA aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa.

13Mche BWANA, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake.[#Mt 4:10; Lk 4:8; Kum 13:4; Zab 63:11]

14Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao;[#Yer 25:6]

15kwani BWANA, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya BWANA, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi.

16Msimjaribu BWANA, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa.[#Kut 17:1-7; Mt 4:7; Lk 4:12; 1 Kor 10:9]

17Zishikeni kwa bidii sheria za BWANA, Mungu wenu, na maagizo yake, na amri zake alizokuagiza.[#Zab 119:4]

18Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa BWANA; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri BWANA aliyowaapia baba zako,

19ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema BWANA.

20Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, Ni nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza BWANA, Mungu wetu?

21Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; BWANA, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu;

22BWANA akaonesha ishara na maajabu makubwa na mazito, juu ya Misri, Farao, na nyumba yake yote, mbele ya macho yetu;

23akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia babu zetu.

24BWANA akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche BWANA, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo.[#Ayu 35:7,8; Yer 32:39; Zab 41:2; Lk 10:28]

25Tena itakuwa haki kwetu, tukizingatia kufanya maagizo haya yote mbele ya BWANA, Mungu wetu, kama alivyotuagiza.[#Rum 10:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya