The chat will start when you send the first message.
1Kuna baa nililoliona mimi chini ya jua, nalo linawalemea wanadamu kwa uzito;
2mtu aliyepewa na Mungu mali, ukwasi, na heshima, hata asipungukiwe na kitu chochote kwa nafsi yake, katika yote anayoyatamani lakini Mungu hamwezeshi kula katika hizo; bali mgeni hula. Hayo ndiyo ubatili hasa, nayo ni ugonjwa mbaya.[#Kum 8:7-10; Amu 18:10; Ayu 21:10; Zab 17:14; Lk 12:19,20]
3Mtu akizaa watoto mia moja, akaishi miaka mingi, hata siku za maisha yake zikiwa nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo;[#2 Fal 9:35; Est 7:10; Isa 14:19; Ayu 3:16; Zab 58:8]
4yaani, hiyo huja katika ubatili, na huenda gizani, nalo jina lake limefunikwa giza;
5tena, haikuliona jua wala kulifahamu; basi, hii imepata kustarehe kuliko yule;
6naam, ajapoishi miaka elfu mara mbili, asijiburudishe kwa mema; je! Wote hawaendi mahali pamoja?
7Juhudi zote za binadamu ni kwa kinywa chake,[#Mit 16:26; 1 Tim 6:6-8]
Lakini hamu yake haitosheleki.
8Kwa maana mwenye hekima hupata faida gani kuliko mpumbavu? Au maskini ana nini kuliko yeye ajuaye kwenda mbele ya walio hai?
9Heri kuona kwa macho,
Kuliko kutangatanga kwa tamaa.
Hayo nayo ni ubatili, na kufukuza upepo.
10Na awe kitu chochote, aliitwa jina lake zamani za kale, naye amejulikana kuwa ndiye mwanadamu; wala hawezi kabisa kushindana na yeye aliye na uwezo kuliko yeye mwenyewe.[#Ayu 9:32; Isa 45:9; Rum 9:19,20]
11Basi, kwa kuwa kuna mambo mengi yaongezayo ubatili, mwanadamu hufaidiwa nini?
12Kwa maana ni nani ajuaye yaliyo mema ya mwanadamu katika maisha yake, siku zote za maisha yake ya ubatili, anayoishi kama kivuli? Kwa maana ni nani awezaye kumweleza mwanadamu mambo yatakayofuata baada yake chini ya jua?[#Yak 4:14; Zab 39:6]