Estk 5

Estk 5

Esta Awaalika Mfalme na Hamani

1Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa kasri.

2Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.

3Mfalme akamwambia, Malkia Esta, unataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.[#Mk 6:23]

4Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.

5Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyoomba. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.

6Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utatimiziwa.

7Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii,

8Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunitimizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.

9Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kunyenyekea mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai.

10Lakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma watu kuwaita marafiki zake na Zereshi mkewe.

11Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, na pia mambo yote ambayo mfalme amemfanikisha kwayo, na jinsi alivyompandisha cheo juu ya wakuu na watumishi wa mfalme.

12Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu yeyote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme.

13Bali haya yote yanifaa nini, niendeleapo kumwona yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme?

14Basi Zereshi mkewe na marafiki wote wa Hamani wakamwambia, Na kitengenezwe kiunzi cha mti wa kunyongea wa urefu wa mikono hamsini, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa furaha pamoja na mfalme karamuni. Basi ushauri huu ukamridhisha Hamani, akautengeneza mti wa kunyongea.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya