The chat will start when you send the first message.
1Kisha akafanya hiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, ya mti wa mshita urefu wake ulikuwa dhiraa tano, na upana wake ulikuwa dhiraa tano, ilikuwa mraba; na kwenda juu kwake kulikuwa dhiraa tatu.[#Kut 27:1; 2 Nya 29:23,24; Zab 51:15-19; Isa 61:8; Eze 44:11; 45:17; Ebr 9:14; 13:10]
2Naye akazifanya pembe zake katika ncha zake nne; hizo pembe zilikuwa za kitu kimoja nayo; naye akaifunika shaba.
3Kisha akafanya vyombo vyote vya madhabahu, yaani sufuria zake, na majembe yake, na mabakuli yake, na uma zake, na meko yake; vyombo vyake vyote akavifanya vya shaba.[#1 Fal 7:45]
4Naye akaifanyia madhabahu wavu wa shaba, akautia chini ya ukingo kuizunguka pande zote, ukawa katikati ya hiyo madhabahu.
5Naye akasubu vikuku vinne kwa kutiwa katika pembe nne za huo wavu wa shaba, viwe mahali pa kutia ile miti ya kuichukulia.
6Naye akaifanya hiyo miti kwa mti wa mshita na kuifunika shaba.
7Naye akaitia ile miti katika vile vikuku vilivyokuwa katika mbavu za hiyo madhabahu, ili kuichukua; akaifanya yenye mvungu ndani, kwa zile mbao.
8Kisha akafanya hilo birika la shaba, na kitako chake cha shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania.[#Kut 30:18; 2 Fal 16:17; 2 Nya 4:2; Zab 26:6; Zek 13:1; Eze 36:25; 2 Kor 7:1; Ebr 10:22; 1 Yoh 5:6]
9Naye akafanya ua; upande wa kusini kwa kuelekea kusini, chandarua cha ua kilikuwa cha nguo ya kitani nzuri ya kusokotwa, kiasi cha dhiraa mia moja;[#Kut 27:9; Zab 84:2; 92:13]
10nguzo zake zilikuwa ishirini, na vitako vyake vilikuwa ishirini, vilikuwa vya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
11Upande wa kaskazini ulikuwa ni dhiraa mia moja vivyo hivyo, nguzo zake ishirini na vitako vyake ishirini, vilikuwa ni vya shaba; kulabu za nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
12Upande wa magharibi mlikuwa na chandarua ya dhiraa hamsini, nguzo zake zilikuwa ni kumi, na vitako vyake kumi; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
13Upande wa mashariki kuelekea mashariki dhiraa hamsini.
14Chandarua ya upande mmoja wa lango ilikuwa dhiraa kumi na tano urefu wake; na nguzo zake tatu, na vitako vyake vitatu;
15ni vivyo hivyo upande wa pili; upande huu na huu langoni mwa ua mlikuwa na chandarua ya dhiraa kumi na tano urefu wake; nguzo zake zilikuwa ni tatu, na vitako vyake vitatu.
16Vyandarua vya nguo zote za ule ua vilivyouzunguka pande zote vilikuwa ni vya kitani nzuri iliyosokotwa.
17Na vitako vya zile nguzo vilikuwa vya shaba; kulabu za hizo nguzo na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha; na vichwa vya zile nguzo vilikuwa ni vya fedha; na nguzo zote za huo ua ziliungwa kwa vitanzi vya fedha.
18Na hilo pazia la lango la ua, lilikuwa ni kazi ya mwenye kutia taraza, lilikuwa la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani nzuri ya kusokotwa; lilikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, na kutukuka kwake katika huo upana wake kulikuwa dhiraa tano, kupatana na ile chandarua ya ua.[#2 Nya 3:14]
19Na nguzo zake zilikuwa nne, na vitako vyake vinne, vilikuwa vya shaba; kulabu zake zilikuwa za fedha, na vichwa vyake na vitanzi vyake vilikuwa vya fedha.
20Na vigingi vyote vya maskani, na vya ua ulioizunguka pande zote vilikuwa vya shaba.[#Kut 27:19; 2 Nya 3:9; Ezr 9:8; Isa 22:23; Efe 2:21,22]
21Jumla ya vile vyombo vilivyofanywa kwa ajili ya hiyo maskani, hiyo maskani ya ushuhuda ni hii, kama vilivyohesabiwa, kama maagizo ya Musa yalivyokuwa, kwa ajili ya utumishi wa Walawi kwa mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni, kuhani.[#Hes 1:50; 9:15; 18:2; 2 Nya 24:6; Mdo 7:44; Hes 4:28,33]
22Na Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, akafanya yote BWANA aliyomwagiza Musa.[#Kut 31:2,6]
23Na pamoja naye alikuwa na Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, aliyekuwa fundi wa kuchora nakshi, mfanyaji wa kazi mwerevu, naye alikuwa mwenye kutia taraza za nyuzi za rangi ya samawati, na za rangi ya zambarau, na nyekundu, na kitani nzuri.
24Dhahabu yote iliyotumiwa kwa ajili ya hiyo kazi, katika kazi hiyo yote ya mahali patakatifu, hiyo dhahabu ya matoleo, ilikuwa ni talanta ishirini na tisa, na shekeli mia saba na thelathini, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu.[#Kut 30:13; Law 5:15; 27:3,25; Hes 3:47; 18:16]
25Na fedha ya hao waliohesabiwa, watu wa huo mkutano ilikuwa talanta mia moja, na shekeli elfu moja na mia saba na sabini na tano kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu;[#Kut 30:11-16]
26kichwa beka, maana, nusu shekeli, kwa kadiri ya shekeli ya mahali patakatifu, kwa ajili ya kila mtu aliyepita kwa wale waliohesabiwa, aliyekuwa wa umri wa miaka ishirini au zaidi, kwa ajili ya wanaume elfu mia sita na tatu mia tano na hamsini (603,550).[#Mt 17:24; Kut 30:13,15; Hes 1:46]
27Na hizo talanta mia moja za fedha zilikuwa kwa kutengenezea vile vitako vya mahali patakatifu na vitako vya hilo pazia; vitako mia moja kwa hizo talanta mia moja, talanta moja kitako kimoja.[#Kut 26:19-32]
28Na kwa hizo shekeli elfu moja na mia saba, na sabini na tano, akafanya vifungo vya hizo nguzo, na kuvifunika fedha vile vichwa vyake, na kufanya vitanzi vyake.
29Na hiyo shaba iliyoletwa ilikuwa ni talanta sabini, na shekeli elfu mbili na mia nne.
30Naye akafanya ya hiyo shaba vitako kwa ajili ya lango la hema ya kukutania, na hiyo madhabahu ya shaba, na ule wavu wa shaba kwa ajili yake na vyombo vyote vya hiyo madhabahu,
31na vitako vya ua kuuzunguka pande zote, na vitako vya lango la huo ua, na vigingi vyote vya maskani, na vigingi vyote vya huo ua uliozunguka pande zote.[#Kut 27:19; 2 Nya 3:9; Ezr 9:8; Isa 22:23; Efe 2:21,22]