Ezekieli 27

Ezekieli 27

Maombolezo juu ya Tiro

1Neno la BWANA likanijia tena, kusema,

2Na wewe, mwanadamu, mfanyie Tiro maombolezo;[#Eze 26:17]

3umwambie Tiro, Ewe ukaaye penye maingilio ya bahari, uliye mchuuzi wa watu wa kabila nyingi, mpaka visiwa vingi, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe, Tiro, umesema, Mimi ni ukamilifu wa uzuri.[#Eze 28:2; Isa 23:3]

4Mipaka yako i kati ya moyo wa bahari; wajenzi wako wameukamilisha uzuri wako.

5Mbao zako zote wamezifanya kwa misonobari itokayo Seniri; wametwaa mierezi ya Lebanoni ili kukufanyia mlingoti;[#Kum 3:9]

6kwa mialoni ya Bashani wamefanya makasia yako; na sitaha zako wamezifanya kwa pembe iliyotiwa kazi ya njumu katika mti wa mihugu itokayo Kitimu.[#Yer 2:10]

7Tanga lako lilikuwa la kitani safi itokayo Misri, iliyotiwa taraza, ili iwe bendera kwako; na chandarua chako kilikuwa cha rangi ya samawati na urujuani toka visiwa vya Elisha.[#Mwa 10:4]

8Wakaao Sidoni na Arvadi ndio waliovuta makasia yako; wana wako wenye akili, Ee Tiro, walikuwa ndani yako, ndio waliokuwa rubani zako.

9Wazee wa Gebali na wenye akili wake walikuwa ndani yako, wenye kutia kalafati; merikebu zote za bahari na mabaharia wao walikuwa ndani yako, ili kubadiliana biashara yako.[#Yos 13:5]

10Watu wa Uajemi na Ludi na Putu walikuwa katika jeshi lako, watu wako wa vita; walitungika ngao na chapeo ndani yako; wakadhihirisha uzuri wako.[#Yer 46:9; Eze 30:5]

11Watu wa Arvadi, pamoja na jeshi lako, walikuwa juu ya kuta zako pande zote, na Wagamadi walikuwa ndani ya minara yako; walitungika ngao zao juu ya kuta zako pande zote; wakaukamilisha uzuri wako.

12Tarshishi alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa utajiri wa kila aina; kwa fedha, na chuma, na bati, na risasi, walifanya biashara, wapate vitu vyako vilivyouzwa.[#2 Nya 20:36]

13Ugiriki na Tubali na Mesheki ndio waliokuwa wachuuzi wako; walitoa wanadamu, na vyombo vya shaba, kwa biashara yako.[#1 Nya 1:5; Yoe 3:6]

14Watu wa nyumba ya Togarma walifanya biashara, kwa farasi, naam, farasi wa vita, na nyumbu, wapate vitu vyako vilivyouzwa.[#Mwa 10:3; 1 Nya 1:6]

15Wadedani walikuwa wachuuzi wako, visiwa vingi vilikuwa soko la mkono wako; walikuletea pembe, na mpingo, ili kuvibadili.[#Mwa 10:7; 1 Nya 1:9]

16Shamu alikuwa mfanya biashara kwako, kwa sababu ya wingi wa kazi za mkono wako walifanya biashara kwa zumaridi, urujuani, kazi ya taraza, kitani safi, marijani na akiki, wapate vitu vyako vilivyouzwa.

17Yuda, na nchi ya Israeli, walikuwa wachuuzi wako; walitoa badala ya bidhaa yako ngano ya Minithi, na mtama, na asali, na mafuta, na zeri.[#1 Fal 5:9; Mdo 12:20]

18Dameski alikuwa mfanya biashara kwako, kwa habari ya wingi wa kazi za mkono wako, kwa ajili ya wingi wa aina zote za utajiri; akaleta divai ya Helboni, na sufu nyeupe.

19Wedani, na Yavani, walifanya biashara toka Uzali kwa vitu vyako; chuma kilichofuliwa, na mdalasini, na mchai, vilikuwa katika bidhaa yako.

20Dedani alikuwa mchuuzi wako, kwa nguo za thamani za kutandikia farasi.[#Mwa 25:3]

21Arabuni, na wakuu wote wa Kedari, ndio waliokuwa wafanya biashara wa mkono wako; kwa wana-kondoo, na kondoo dume, na mbuzi; kwa hao walifanya biashara nawe.[#Mwa 25:13; 1 Nya 1:29]

22Wachuuzi wa Sheba, na Raama, ndio waliokuwa wachuuzi wako; badala ya vitu vyako walitoa manukato yaliyo mazuri, na kila aina ya vito vya thamani, na dhahabu.[#Mwa 10:7; Zab 72:10,15; Isa 60:6]

23Harani, na Kane, na Adini, wachuuzi wa Sheba, na Ashuru, na Kilmadi, walikuwa wachuuzi wako.[#Mwa 11:31; 25:3; 2 Fal 19:12; Mdo 7:4]

24Hao ndio waliokuwa wachuuzi wako, kwa vitu vya tunu, kwa vitumba vya nguo za samawati na kazi ya taraza, na masanduku ya mavazi ya thamani, yaliyofungwa kwa kamba, na kufanyizwa kwa mti wa mierezi, katika bidhaa yako.

25Merikebu za Tarshishi zilikuwa misafara yako, kwa bidhaa yako; nawe ulijazwa sana, ukawa mtukufu sana, katika moyo wa bahari.[#Isa 2:16; Ufu 18:11-19]

26Wavuta makasia wako walikuleta katika maji makuu; upepo wa mashariki umekuvunja moyoni mwa bahari.[#Zab 48:7]

27Mali zako, na bidhaa yako, na utajiri wako, wanamaji wako, na rubani zako, na wenye kutia kalafati wako, na wafanya biashara wako, na watu wako wa vita wote, walio ndani yako, pamoja na jeshi lako lote lililo ndani yako, wataanguka katika moyo wa bahari katika siku ya kuangamia kwako.[#Mit 11:4]

28Kwa sauti ya vilio vya rubani zako viunga vyako vitatetemeka.

29Na wote wavutao kasia, wanamaji, na rubani zote wa baharini, watashuka katika merikebu zao, na kusimama katika nchi kavu;[#Ufu 18:17]

30nao wataomboleza kwa sauti juu yako, nao watalia kwa uchungu, na kutupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na kugaagaa katika majivu;[#Neh 9:1; Omb 2:10; Ufu 18:19; Est 4:1]

31nao watajifanya kuwa na upaa kwa ajili yako, na kujifunga nguo za magunia viunoni, nao watakulilia kwa uchungu wa roho, kwa maombolezo ya uchungu.

32Na katika kulia kwao watakufanyia maombolezo, na kukuombolezea, wakisema, Ni nani aliye kama Tiro, kama yeye aliyenyamazishwa kati ya bahari?

33Bidhaa zako zilipotoka katika bahari, uliwajaza watu wa kabila nyingi; uliwatajirisha wafalme wa dunia, kwa wingi wa mali zako, na kwa utajiri wako.

34Wakati ulipovunjwa na bahari, katika vilindi vya maji, bidhaa zako na jeshi lako lote walianguka kati yako.

35Wote wakaao katika visiwa vile watakustaajabia, na wafalme wao wameogopa sana, wamefadhaika nyuso zao.[#Eze 26:15]

36Wafanya biashara kati ya makabila ya watu wakuzomea; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena milele.[#Yer 18:16]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya