Ezekieli 34

Ezekieli 34

Wachungaji waongo wa Israeli

1Neno la BWANA likanijia, kusema,

2Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?[#Eze 33:24; Yer 23:1]

3Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.[#Isa 56:11; Mik 3:3]

4Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala.[#Zek 11:16; 2 Tim 2:24; Lk 15:4; 1 Pet 5:3; Mt 9:36; Isa 56:9]

5Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyamamwitu, wakatawanyika.[#Hes 27:17; 1 Fal 22:17; Mt 9:36; Mk 6:34]

6Kondoo wangu walitangatanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta.

7Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA;

8Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo wangu walikuwa mateka, kondoo wangu wakawa chakula cha wanyamamwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo wangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo wangu;

9kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA;

10Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo wangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo wangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.[#Eze 3:18; 33:6-8; Ebr 13:17]

11Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo wangu, na kuwatunza.

12Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo wake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo wake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.[#Yer 13:16; Eze 30:3; Yoe 2:2; Sef 1:15; Mdo 2:19-21]

13Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.[#Isa 65:9,10; Yer 23:3; 36:24]

14Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.[#Zab 23:2; 34:8-10; Isa 25:6; 30:23,24; Yer 31:12-14,25; Yn 10:9; Yer 33:12]

15Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.

16Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliotangatanga, nitawatibu waliojeruhiwa, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.[#Isa 40:11; 61:1-3; Mik 4:6,7; Mt 15:24; Mk 2:17]

17Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo dume na mbuzi dume pia.[#Eze 20:37; Zek 10:3; Mt 25:32]

18Je! Mwaona ya kuwa ni neno dogo ninyi kulishwa malisho mema, hata mkawa hamna budi kukanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia? Na kuwa mmekunywa maji yaliyo safi, nanyi hamna budi kuyatibua kwa miguu yaliyobaki?[#Mt 23:13]

19Na kwa habari za kondoo wangu, wao wanakula hayo mliyoyakanyaga kwa miguu yenu, nao wanakunywa maji mliyoyatibua kwa miguu yenu.

20Kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU awaambia hivi; Tazama, mimi, naam, mimi, nitahukumu kati ya wanyama walionona na wanyama waliokonda.

21Kwa kuwa mmesukuma kwa ubavu, na kwa mabega, na kuwapiga wenye maradhi kwa pembe zenu, hata mkawatawanyia mbali;

22basi mimi nitaliokoa kundi langu, wala hawatakuwa mateka tena; nami nitahukumu kati ya mnyama na mnyama.

23Nami nitaweka mchungaji mmoja juu yao, naye atawalisha, naam, mtumishi wangu, Daudi; yeye atawalisha, naye atakuwa mchungaji wao.[#Isa 40:11; Yn 10:11; Ebr 13:20; Yer 30:9; Eze 37:24]

24Na mimi, BWANA, nitakuwa Mungu wao, na mtumishi wangu, Daudi, atakuwa mkuu kati yao; mimi, BWANA, nimesema haya.[#Mwa 17:7; Kut 29:45; Lk 1:32]

25Nami nitafanya agano la amani nao, nami nitawakomesha wanyama wakali kati yao; nao watakaa salama jangwani, na kulala misituni.[#Law 26:6; Isa 11:6; Yer 23:6]

26Nami nitawafanya wao, na mahali palipo pande zote za mlima wangu, kuwa baraka, nami nitaleta manyunyu kwa wakati wake; yatakuwako manyunyu ya baraka.[#Isa 56:7; Mwa 12:2; Law 26:4; Zab 68:9; Mal 3:10]

27Na mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, nao watakuwa salama katika nchi yao; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA, nitakapovunja vifungo vya nira zao, na kuwaokoa katika mikono ya watu wale waliowatumikisha.[#Zab 85:12; Yer 2:20; 25:14]

28Hawatakuwa mateka ya mataifa tena, wala mnyama wa nchi hatawala; bali watakaa salama salimini, wala hapana mtu atakayewatia hofu.[#Eze 36:4]

29Nami nitawainulia miche iwe sifa njema, wala hawataangamizwa kwa njaa katika nchi yao tena, wala hawatatukanwa tena na mataifa.

30Nao watajua ya kuwa mimi, BWANA, Mungu wao, ni pamoja nao, na ya kuwa wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana MUNGU.[#2 Tim 1:12]

31Na ninyi, kondoo wangu, kondoo wa malisho yangu, ni wanadamu, na mimi ni Mungu wenu, asema Bwana MUNGU.[#Zab 100:3]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya