The chat will start when you send the first message.
1Kisha akanirudisha kwa njia ya lango lile la nje, la mahali patakatifu lililoelekea upande wa mashariki; nalo lilikuwa limefungwa.[#Eze 43:1]
2BWANA akaniambia, Lango hili litafungwa, halitafunguliwa, wala mtu awaye yote hataingia kwa lango hili, kwa maana BWANA, Mungu wa Israeli, ameingia kwa hilo; basi kwa sababu hiyo litafungwa.
3Na mkuu, yeye ndiye atakayeketi ndani yake ale chakula mbele za BWANA; ataingia kwa njia ya ukumbi wa lango, naye atatoka kwa njia iyo hiyo.[#Zek 6:12; Flp 2:8; Mwa 31:54; Eze 46:2,8]
4Kisha akanileta, kwa njia ya lango la upande wa kaskazini, mbele ya nyumba; nikaangalia, na tazama, huo utukufu wa BWANA uliijaza nyumba ya BWANA; nikaanguka kifudifudi.[#Eze 3:23; 1:28]
5BWANA akaniambia, Mwanadamu, weka moyoni mwako, ukatazame kwa macho yako, ukasikie kwa masikio yako, maneno yote nitakayokuambia, katika habari ya kawaida zote za nyumba ya BWANA, na ya amri zake zote; nawe weka moyoni mwako maingilio ya nyumba, pamoja na matokeo yote ya mahali patakatifu.[#Eze 40:4]
6Nawe utawaambia waasi, yaani nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Enyi nyumba ya Israeli, machukizo yenu yote, na yakome,[#Eze 2:5; 1 Pet 4:3]
7kuwa mmewaingiza wageni, ambao mioyo yao haikutahiriwa, wala miili yao haikutahiriwa, wawe ndani ya patakatifu pangu, wapatie unajisi, naam, nyumba yangu, mtoapo sadaka ya chakula changu, mafuta na damu; nao wameyavunja maagano yangu, juu ya machukizo yenu yote.[#Mdo 21:28; Eze 7:20; Law 26:41; 21:6; 3:16]
8Wala hamkuvilinda vitu vyangu vitakatifu bali mmejiwekea walinzi wa maagizo yangu, katika patakatifu pangu.[#Law 22:2; Hes 18:3; 2 Tim 4:1]
9Bwana MUNGU asema hivi; Hapana mgeni, ambaye moyo wake haukutahiriwa, wala mwili wake haukutahiriwa, atakayeingia patakatifu pangu, miongoni mwa wageni walio kati ya wana wa Israeli.[#Zab 50:16]
10Lakini Walawi waliofarakana nami, wakapotea na kuvifuata vinyago vyao, hapo Waisraeli walipopotea, watachukua uovu wao wenyewe.[#2 Fal 23:8; Neh 9:34; Yer 23:11; Eze 22:26]
11Hata hivyo watakuwa wahudumu katika patakatifu pangu, wakiwa wasimamizi wa malango ya nyumba, wakihudumu humo nyumbani; watawachinjia watu sadaka za kuteketezwa na dhabihu, nao watasimama mbele yao ili kuwahudumia.[#1 Nya 26:1; Hes 16:9]
12Kwa sababu waliwahudumia mbele ya vinyago vyao, wakawa kwazo la uovu kwa nyumba ya Israeli; basi nimeuinua mkono wangu juu yao, asema Bwana MUNGU, nao watachukua uovu wao.[#Zab 106:26]
13Wala hawatanikaribia, kunihudumia katika kazi ya ukuhani, wala hawatakaribia vitu vyangu vitakatifu kimojawapo, vitu vilivyo vitakatifu sana; bali watachukua aibu yao, na machukizo yao yote waliyoyatenda.[#Hes 18:3; Eze 32:30]
14Lakini nitawafanya kuwa walinzi katika ulinzi wa nyumba, kwa huduma yake yote, na kwa yote yatakayotendeka ndani yake.[#1 Nya 23:28,32]
15Lakini makuhani Walawi, wana wa Sadoki, waliosimamia patakatifu pangu, hapo wana wa Israeli walipopotea na kuniacha, hao ndio watakaonikaribia ili kunihudumia; nao watasimama mbele zangu, kunitolea mafuta na damu, asema Bwana MUNGU;[#Eze 40:46; 1 Sam 2:35; Kum 10:8]
16wataingia patakatifu pangu, nao wataikaribia meza yangu, ili kunihudumia, nao watafuata maagizo yangu.[#Eze 41:22; Mal 2:7]
17Itakuwa, hapo watakapoingia kwa malango ya ua wa ndani, watavikwa mavazi ya kitani; wala sufu haitakuwa juu yao, maadamu wanahudumu katika malango ya ua wa ndani, na ndani ya nyumba.[#Kut 28:39-43; Law 16:4]
18Watakuwa na vilemba vya kitani juu ya vichwa vyao, nao watakuwa na suruali za kitani viunoni mwao; hawatajifunga kiunoni kitu kisababishacho jasho.
19Nao watakapotoka kuingia ua wa nje, yaani, ua wa nje wa watu, ndipo watakapoyavua mavazi yao waliyovaa katika huduma yao, na kuyaweka katika vile vyumba vitakatifu, nao watavaa mavazi mengine, wasije wakawatakasa watu kwa mavazi yao.[#Eze 42:14; Kut 29:37; Law 16:23]
20Hawatanyoa vichwa vyao, wala hawataacha nywele zao kuwa ndefu sana; watazipunguza nywele za vichwa vyao tu.[#Isa 28:7; Law 21:5]
21Wala kuhani awaye yote hatakunywa mvinyo, aingiapo katika ua wa ndani.[#Lk 1:15; 1 Tim 3:3; Law 10:9]
22Wala hawataoa wanawake wajane, wala mwanamke aliyeachwa na mume wake; lakini watatwaa mabikira wa wazao wa nyumba ya Israeli, au mjane aliyefiwa na mumewe kuhani.[#Law 21:7,13-14]
23Nao watawafundisha watu wangu tofauti iliyoko kati ya vitu vitakatifu na vitu vya kawaida, na kuwafundisha kupambanua kati ya yaliyo machafu na yaliyo safi.[#Mal 2:7; Law 10:10]
24Na katika mabishano watasimama ili kuamua; wataamua kulingana na hukumu zangu; nao watazishika sheria zangu, na amri zangu, katika sikukuu zangu zote zilizoamriwa; nao watazitakasa sabato zangu.[#Kum 17:8; 1 Tim 4:12; Eze 22:26]
25Wala hawatakaribia maiti na kujitia unajisi; ila kwa ajili ya baba, au mama, au mtoto wa kiume, au wa kike, au ndugu mwanamume, au ndugu mwanamke asiyeolewa bado, waweza kujitia unajisi.[#Law 21:1-4]
26Naye akiisha kutakaswa watamhesabia siku saba.[#Hes 6:10]
27Na katika siku atakayoingia ndani ya patakatifu, katika ua wa ndani, ili kuhudumu ndani ya patakatifu, atatoa sadaka yake ya dhambi, asema Bwana MUNGU.[#Law 4:3]
28Nao watakuwa na urithi; mimi ni urithi wao; wala hamtawapa milki iwayo yote katika Israeli; mimi ni milki yao.[#Kum 10:9; Yos 13:14,33; Eze 45:4; Hes 18:20]
29Wataila sadaka ya unga, na sadaka ya dhambi, na sadaka ya hatia, na kila kitu katika Israeli kilichowekwa wakfu kitakuwa chao.[#Law 6:18; Hes 18:8-19]
30Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi, ili kuleta baraka juu ya nyumba yako.[#Hes 15:20; Mit 3:9]
31Makuhani hawatakula nyamafu, au iliyoraruliwa, ikiwa ya ndege au ya mnyama.[#Kut 22:31; Law 22:8]