Mwanzo 31

Mwanzo 31

Yakobo atoroka na jamaa na mifugo wake

1Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.[#Ayu 5:2; 31:31; Zab 57:4; Rum 13:13; Tit 3:3; Yak 3:8; Zab 49:16]

2Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama hapo awali.[#Mwa 4:5; Kum 28:54]

3BWANA akamwambia Yakobo, Urudi katika nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.[#Mwa 28:15; 32:9]

4Yakobo akatuma watu ili kuwaita Raheli na Lea waje malishoni kwenye mifugo wake. Akawaambia,

5Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama hapo awali. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.[#Mwa 21:22; Isa 41:10; Ebr 13:5]

6Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu.[#Mwa 30:29]

7Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwachia anidhuru.[#Mwa 15:1; 20:6; Ayu 22:25; Zab 5:11; 7:10; Mit 30:5]

8Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.[#Mwa 30:32]

9Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.[#Mwa 31:16]

10Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, niliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.

11Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.[#Mwa 48:16]

12Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda kondoo wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutenda Labani.[#Kut 3:7; Kum 24:15; Zab 12:5; Efe 6:9]

13Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa.[#Mwa 28:18-22; 32:9]

14Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je, Imebakia sehemu au urithi kwa ajili yetu katika nyumba ya baba yetu?[#Mwa 2:24]

15Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?[#Amu 17:5; 1 Sam 19:13; Eze 21:21; Hos 3:4]

16Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi, yoyote Mungu aliyokuambia, uyafanye.

17Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia.

18Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa amepata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani.

19Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye.[#Mwa 35:2]

20Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.

21Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, na kuelekea kwenye nchi ya milima ya Gileadi.[#Mwa 46:28; 2 Fal 12:17; Lk 9:51]

Labani amfuatilia Yakobo

22Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia,

23akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi.[#Mwa 13:8]

24Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.[#Mwa 20:3; Ayu 33:15; Mt 1:20; Mwa 24:50]

25Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika nchi ya milima ya Gileadi.

26Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga.[#1 Sam 30:2]

27Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi?

28Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.[#Rut 1:9; 1 Fal 19:20; Mdo 20:37; 1 Sam 13:13; 2 Nya 16:9]

29Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.[#Mwa 28:13; Zab 5:11; 84:11; 115:9]

30Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu?[#Mwa 31:19; Yos 24:2; Amu 18:24; Mdo 19:26]

31Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu niliogopa, nikasema, Usije ukaninyang'anya binti zako kwa nguvu.

32Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli ameiiba.[#Mwa 44:9]

33Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia katika hema ya Raheli.[#Mwa 44:9]

34Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona.

35Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago.[#Kut 20:12; Law 19:32; Efe 6:1]

36Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Ni nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata ukanifuatia namna hii?[#Efe 4:26]

37Umepekua vyombo vyangu vyote; ni kitu gani ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu zako, wakaamue kati yetu.[#1 Sam 12:3; 1 Kor 6:5]

38Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo wako wala mbuzi wako wa kike hawakuharibu mimba wala wa kiume katika wanyama wako sikuwala.

39Kilichoraruliwa na mnyama wa porini sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, kiwe kilichukuliwa mchana au kilichukuliwa usiku.[#Kut 22:10,12]

40Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu.

41Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi.[#Mwa 29:27; 31:7]

42Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Abrahamu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu.[#Zab 124:1; Isa 8:13; Kut 3:7; 1 Nya 12:17]

Labani na Yakobo wawekeana agano

43Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea?

44Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.[#Mwa 26:28; Yos 24:27]

45Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo.[#Mwa 28:18]

46Yakobo akawaambia ndugu zake, Kusanyeni mawe. Wakatwaa mawe, wakafanya chungu, nao wakala huko karibu na ile chungu.

47Labani aliiita Yegarsahadutha, lakini Yakobo aliiita Galedi.

48Labani akasema, Chungu hii ni shahidi kati ya mimi na wewe hivi leo. Kwa hiyo likaitwa jina lake Galedi,[#Yos 24:27]

49na Mispa, maana alisema, Mungu avizie kati ya mimi na wewe, wakati tusipoonana.[#Amu 11:29; 1 Sam 7:5]

50Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe.

51Labani akamwambia Yakobo, Tazama rundo hili la mawe haya utazame na nguzo niliyoisimika kati ya mimi na wewe.

52Chungu hii na iwe shahidi, na nguzo hii na iwe shahidi, ya kuwa mimi sitapita chungu hii kuja kwako, wala wewe hutapita chungu hii na nguzo hii uje kwangu, kwa madhara.

53Mungu wa Abrahamu, na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba yao, ahukumu kati yetu.[#Mwa 16:5; 21:23]

Yakobo akaapa kwa Hofu ya Isaka baba yake.

54Yakobo akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani.

55Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.[#Mwa 28:1; 2 Sam 6:20]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya