The chat will start when you send the first message.
1Njaa ikawa kali katika nchi.[#Mwa 12:10; 26:1; 41:57; 1 Fal 18:2; 2 Fal 8:1; Yer 52:6]
2Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo.
3Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi.[#Mwa 42:20; 44:23]
4Ukimtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula.
5Ila usipomtuma, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi.
6Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine?
7Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tungaliwezaje kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu?
8Yuda akamwambia Israeli baba yake, Mtume kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu.
9Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima;[#Mwa 44:32; Flm 1:18,19]
10maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili.
11Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi.[#Mwa 32:20; 37:25; Mit 18:16; Yer 8:22; Eze 27:17]
12Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa.[#Mwa 42:25,35]
13Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule.
14Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.[#1 Sam 14:6; 2 Sam 22:3,31; Ayu 13:15; Zab 22:4; 34:8,22; Mit 28:5; Isa 57:13; Nah 1:7]
15Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu.
16Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje mnyama na kuwaandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri.[#Mwa 24:2; 39:4]
17Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu.
18Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutushika, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda wetu.
19Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba.
20Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula.
21Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu.[#Mwa 42:27,35]
22Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu.
23Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu zilinifikia. Kisha akawatolea Simeoni kwao.
24Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakanawa miguu, akawapa punda wao chakula.[#Mwa 18:4; 24:32; Lk 7:44; Yn 13:5; 1 Tim 5:10]
25Wakaiweka tayari ile zawadi hadi atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko.
26Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka chini.[#Mwa 27:29; 33:6; Rut 2:10]
27Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai?[#Mwa 42:11-13]
28Wakasema, Mtumishi wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu.[#Mwa 37:7,10; Mit 14:19]
29Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mama yake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu.[#Mwa 35:17,18; 42:13]
30Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulilia, akaingia chumbani mwake, akalilia humo.[#1 Fal 3:26; Yer 31:20; Mwa 42:24; 2 Sam 18:33]
31Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula.[#Mwa 43:25]
32Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri.[#Mwa 46:34; Kut 8:26]
33Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa haki ya uzawa wake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao.
34Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafurahi pamoja naye.[#Mwa 45:22]