Mwanzo 50

Mwanzo 50

1Yusufu akamwangukia babaye usoni, akamlilila, akambusu.[#Mwa 46:4; 2 Fal 13:14]

2Yusufu akawaagiza watumishi wake waganga wampake baba yake dawa asioze. Waganga wakampaka dawa Israeli.[#2 Nya 16:14; Mt 26:12; Mk 14:8; 16:1; Lk 24:1; Yn 19:39,40]

3Siku zake arubaini zikaisha, maana siku hizo zilitimiza siku za wale waliohifadhiwa kwa kupakwa dawa. Wamisri wakamwombolezea siku sabini.[#Hes 20:29; Kum 34:8]

4Siku za kumwombolezea zilipopita, Yusufu alisema na watu wa nyumba ya Farao, akinena, Kama nimeona neema machoni penu, tafadhalini mkaseme masikioni mwa Farao, mkinena, Baba yangu aliniapisha, akisema,[#Est 4:2]

5Mimi ni katika kufa, unizike katika kaburi langu nililojichimbia katika nchi ya Kanaani. Basi tafadhali uniruhusu niende sasa nikamzike babangu, nami nitarudi.[#2 Nya 16:14; Isa 22:16; Mt 27:60]

6Farao akasema, Nenda, ukamzike baba yako, kama alivyokuapisha.

7Basi Yusufu akaenda kumzika baba yake, na watumishi wote wa Farao wakaenda pamoja naye, wazee wa nyumbani mwake, na wazee wote wa nchi ya Misri.

8Na nyumba yote ya Yusufu, na ndugu zake, na nyumba ya baba yake; wakawaacha watoto wao tu, na kondoo wao, na ng'ombe wao, katika nchi ya Gosheni.

9Kisha wakaenda pamoja naye wapanda farasi, na magari; wakawa jeshi kubwa sana.

10Wakaja mpaka uwanja wa kupuria nafaka wa Atadi, uliyo ng'ambo ya Yordani. Wakaomboleza huko maombolezo makuu, mazito sana. Akafanya matanga ya baba yake siku saba.[#Mdo 8:2; 1 Sam 31:13; Ayu 2:13]

11Nao waliokaa katika nchi, wale Wakanaani, walipoyaona matanga katika sakafu ya Atadi, wakasema, Matanga haya ya Wamisri ni makuu kwa hiyo mahali pale paliitwa Abel-Misri, iliyo ng'ambo ya Yordani.

12Wanawe wakamfanyia kama alivyowaagiza;

13kwa kuwa wanawe wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, na wakamzika katika pango ya shamba la Makpela, iliyo mbele ya Mamre, aliyoinunua Abrahamu pamoja na shamba kwa Efroni Mhiti, pawe milki yake ya kuzikia.[#Mwa 23:16; Mdo 7:16]

14Yusufu akarudi Misri, yeye na ndugu zake, na wote waliokwenda pamoja naye kumzika baba yake, baada ya kumzika baba yake.

Yusufu awasamehe ndugu zake

15Ndugu zake Yusufu walipoona ya kwamba baba yao amekufa, walisema, Labda Yusufu atatuchukia; naye atatulipa maovu yetu tuliyomtenda.[#Ayu 15:21]

16Wakatuma watu kwa Yusufu, kunena, Baba yako alitoa amri kabla ya kufa kwake, akasema,

17Mwambieni Yusufu hivi, Naomba uwasamehe ndugu zako kosa lao na dhambi yao, maana walikutenda mabaya; sasa twakuomba utusamehe kosa la watumishi wa Mungu wa baba yako. Yusufu akalia waliposema naye.[#Mit 28:13; Mwa 49:25]

18Ndugu zake wakaenda tena, wakamwangukia miguu, wakasema, Tazama, sisi tu watumishi wako.[#Mwa 37:7,10]

19Yusufu akawaambia, Msiogope, je! Mimi ni badala ya Mungu?[#Kum 32:35; Rum 12:19; Ebr 10:30]

20Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.[#Zab 56:5; Isa 10:7; Mwa 45:5,7; Mdo 3:13-15]

21Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema.[#Mwa 47:12; Mt 5:44]

Siku za mwisho za Yusufu na kifo chake

22Yusufu Akakaa katika Misri, yeye na nyumba ya baba yake. Yusufu Akaishi miaka mia moja na kumi.

23Yusufu akaona wana wa Efraimu hata kizazi cha tatu; na wana wa Makiri, mwana wa Manase, walizaliwa magotini mwa Yusufu.[#Ayu 42:16; Mwa 30:3]

24Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ninakufa, lakini Mungu atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Abrahamu, na Isaka, na Yakobo.[#Kut 8:16,17; Ebr 11:22; Mwa 26:3]

25Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka Mungu atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu.[#Mwa 47:29; Kut 13:19; Yos 24:32]

26Basi Yusufu akafa, mwenye miaka mia moja na kumi; wakampaka dawa, wakamtia katika sanduku, huko Misri.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya