Mwanzo 6

Mwanzo 6

Uovu wa wanadamu

1Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,[#Ayu 1:6; 2:1]

2wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua.[#2 Kor 6:18; Kum 7:3,4]

3BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni mwili; basi siku zake zitakuwa miaka mia moja na ishirini.[#Lk 19:42; Gal 5:16,17; 1 Pet 3:20; Zab 78:39]

4Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa.[#Hes 13:33; #6:4 maana yake ni majitu.]

5BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote.[#Rum 1:28-31; Mwa 8:21; Kum 29:19; Mit 6:18; Mt 15:19; Mt 24:37; Lk 17:26; 1 Pet 3:20]

6BWANA akaghairi kwa kuwa amemwumba mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.[#Hes 23:19; 1 Sam 15:11,29; Isa 63:10; Efe 4:30]

7BWANA akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewaumba.

8Lakini Nuhu akapata neema machoni pa BWANA.[#Mwa 19:19; Kut 33:12; Lk 1:30; Mdo 7:46]

Nuhu atengeneza safina

9Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu.[#2 Pet 2:5]

10Nuhu akazaa wana watatu wa kiume, Shemu, na Hamu, na Yafethi.

11Dunia ikaharibika mbele za Mungu, dunia ikajaa dhuluma.

12Mungu akaiona dunia, na tazama, imeharibika; maana kila mtu duniani amepotoka.[#Zab 14:2; 33:13]

13Mungu akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila kiumbe umefika mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia maovu, basi nitawaangamiza pamoja na dunia.[#Eze 7:2; Amo 8:2; 1 Pet 4:8]

14Jitengenezee safina ya mti wa mvinje; tengeneza vyumba ukaifunike kwa lami ndani na nje.

15Hivi ndivyo utakavyoifanya; dhiraa mia tatu urefu wa safina, dhiraa hamsini upana wake, na dhiraa thelathini kwenda juu.

16Uifanyie safina mwangaza, ukaumalize juu kiasi cha mkono mmoja; ukautie mlango wa safina katika ubavu wake; ukaifanyie dari tatu, ya chini, ya pili, na ya tatu.

17Tazama, nitaleta gharika ya maji juu ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa.[#2 Pet 2:5; Rum 5:12,14]

18Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za wanao, pamoja nawe.

19Na katika kila kilicho hai chenye mwili, wawili wa kila namna utawaleta ndani ya safina, kuwahifadhi pamoja nawe; wawe mume na mke.

20Katika vyote virukavyo kwa jinsi yake, na kila namna ya mnyama kwa jinsi yake, kila kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake, wawili wa kila namna watakuja kwako ili uwahifadhi.

21Ukajitwalie chakula cha kila namna kinacholika, ukakusanye, nacho kitakuwa ni chakula chenu na chao.[#Mwa 1:29,30]

22Ndivyo alivyofanya Nuhu, sawasawa na vyote alivyomwamuru Mungu, hivyo ndivyo alivyofanya.[#Ebr 11:7; Mwa 7:5]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya