The chat will start when you send the first message.
1Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu,[#Ebr 4:14]
2aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.[#Hes 12:7]
3Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba.
4Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.
5Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye;[#Hes 12:7]
6bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya tumaini letu mpaka mwisho.[#Efe 2:19; Kol 1:23]
7Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu,[#Zab 95:7-11]
Leo, kama mkisikia sauti yake,
8Msifanye mioyo yenu kuwa migumu,[#Kut 17:7; Hes 20:2-5]
Kama wakati wa kuasi,
Siku ya kujaribiwa katika jangwa,
9Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima,
Wakaona matendo yangu miaka arubaini.
10Kwa hiyo nilichukizwa na kizazi hiki,
Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa;
Hawakuzijua njia zangu;
11Kama nilivyoapa kwa hasira yangu,[#Hes 14:21-23]
Hawataingia rahani mwangu.
12Hadharini, ndugu zangu, usiwepo katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutoamini, ujitengao na Mungu aliye hai.
13Lakini mwonyane kila siku, maadamu inaitwa leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.[#1 The 5:11]
14Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;[#Ebr 6:11; 11:1]
15kama inenwavyo,[#Zab 95:7-8]
Leo, kama mkisikia sauti yake,
Msifanye mioyo yenu kuwa migumu,
Kama wakati wa kuasi.
16Maana ni akina nani walioasi, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?[#Hes 14:1-35; Kut 17:1]
17Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arubaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?[#Hes 14:29; 1 Kor 10:10]
18Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika pumziko lake, ila wale walioasi?[#Hes 14:22,23]
19Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutoamini kwao.