Isaya 38

Isaya 38

Kuugua kwa Hezekia

1Siku hizo Hezekia aliugua, akawa karibu kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.[#2 Fal 20:1; 2 Nya 32:24]

2Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,

3akasema, Ee BWANA, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia kwa uchungu.[#Neh 5:19]

4Ikawa, neno la BWANA likamjia Isaya, kusema,

5Nenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.

6Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, kutoka kwa mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.[#Isa 37:35]

7Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa BWANA, ya kuwa BWANA atalitimiza jambo hili alilolisema;[#2 Fal 20:8; Isa 37:30]

8Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

9Haya ndiyo maandiko ya Hezekia, mfalme wa Yuda, alipokuwa mgonjwa, naye akapona ugonjwa wake.

10Nilisema, Katika usitawi wa siku zangu nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;[#Zab 102:24]

Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

11Nilisema, Sitamwona BWANA, yeye BWANA, katika nchi ya walio hai;[#Ayu 35:14; Zab 27:13; 31:22; 116:9]

Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao wakaao duniani.

12Makao yangu yameondolewa kabisa,[#Ayu 7:6; 2 Kor 5:4; Zab 102:11,23,24]

yamechukuliwa kama hema ya mchungaji;

Nimekunja maisha yangu kama mfumaji;

atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;

Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

13Nilijituliza hata asubuhi;

kama simba, anaivunja mifupa yangu yote;

Tangu mchana hata usiku wanimaliza.

14Kama mbayuwayu au korongo ndivyo nilivyolia;[#Isa 59:11]

Niliomboleza kama hua;

macho yangu yamedhoofu kwa kutazama juu;

Ee BWANA, nimeonewa, na uwe mdhamini wangu.

15Niseme nini? Yeye amenena nami,[#Ayu 7:11]

na yeye mwenyewe ametenda hayo;

Nitakwenda polepole miaka yangu yote,

kwa sababu ya uchungu wa nafsi yangu.

16Ee Bwana, kwa mambo hayo watu huishi;

Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote;

Kwa hiyo uniponye na kunihuisha.

17Tazama; nilikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu;

Lakini kwa kunipenda umeniokoa kutoka kwa shimo la uharibifu;

Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako.

18Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu;[#Zab 6:5; 30:9; Mhu 9:10]

mauti haiwezi kukuadhimisha;

Wale washukao shimoni hawawezi kuutumainia uaminifu wako.

19Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo;[#Kum 4:9; Zab 78:3]

Baba atawajulisha watoto uaminifu wako.

20BWANA yu tayari kunipa wokovu.[#Zab 9:13; 46:1; 66:12]

Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu,

Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa BWANA.

21Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.[#2 Fal 20:7]

22Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa BWANA?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya