Isaya 46

Isaya 46

1Beli anaanguka chini, Nebo anainama; sanamu zao ziko juu ya wanyama, na juu ya ng'ombe; vitu vile mlivyokuwa mkivichukua huku na huku vimekuwa mzigo, mzigo wa kumlemea mnyama aliyechoka.[#Yer 51:44; 10:5]

2Wanajiinamisha, wanainama pamoja; hawakuweza kuutua mzigo, bali wao wenyewe wamekwenda kufungwa.

3Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani;[#Kut 19:4; Kum 1:31]

4na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.[#Zab 102:27; Mal 3:6; Zab 48:14]

5Mtanifananisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawasawa?

6Watu wamwagao dhahabu kutoka mfukoni, na kupima fedha katika mizani, huajiri mfua dhahabu, akaifanya mungu; huanguka, naam, huabudu.

7Humchukua begani, humchukua, wakamsimamisha mahali pake, akasimama; hataondoka katika mahali pake, naam, mmoja atamwita, lakini hawezi kujibu, wala kumwokoa kutoka kwa taabu yake.[#Yer 10:5]

8Kumbukeni haya, mkajioneshe kuwa wanaume; jifahamisheni haya, ninyi mkosao;

9kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi;[#Kum 32:7]

10nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.[#Zab 33:11; Mit 19:21; Mdo 5:39; Ebr 6:17]

11Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam, nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya.[#Hes 23:19; Tit 1:2]

12Nisikilizeni, ninyi mlio na moyo mshupavu, mlio mbali na haki;[#Rum 10:3]

13Mimi ninaleta karibu haki yangu, haitakuwa mbali, na wokovu wangu hautakawia; nami nitaweka wokovu katika Sayuni kwa ajili ya Israeli, utukufu wangu.[#Rum 1:17; Isa 56:1; Hab 2:3; Mt 3:2; Lk 19:10; Mdo 13:36; 1 Tim 1:15; Isa 62:11; Zek 9:9]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya