Yudithi 10

Yudithi 10

YUDITHI NA HOLOFENE

Yudithi ajiandaa kumwendea Holofene

1Ikawa, alipokwisha kumlilia Mungu wa Israeli, na kuyamaliza maneno hayo yote,

2aliondoka chini, akamwita mjakazi wake, akashuka kwenda nyumbani alimozoea kukaa katika sabato na sikukuu zake,

3akalivua gunia alilovikwa, na mavazi ya ujane wake, akaoga maji mwili wote, akajipaka marhamu mazuri, akasuka nywele akazipamba. Akavaa nguo zake za furaha, ndizo zile alizozivaa alipokuwa hai mumewe Manase.

4Akachukua viatu vya miguu yake, akavaa mikufu yake, na vikuku vyake, na pete zake, na vipuli vyake, na mapambo yake yote, akajipamba vizuri sana, kwa jinsi ya kuvuta macho ya watu wote watakaomwona.

5Akampa mjakazi wake kiriba cha divai na chupa ya mafuta, akajaza mfuko bisi na tini na mikate safi; akafunganya vyombo vyake vyote, akampa.

6Wakaenda mpaka mlango wa mji wa Bethulia, wakawakuta Uzia na wakuu wa mji, Chabrisi na Charmisi, wamesimama pale.

7Nao walipomwona, jinsi sura yake ilivyogeuka na nguo zake zikabadilika, walistaajabu sana kwa uzuri wake, wakamwambia,

8Mungu wa baba zetu akauoneshe kibali, na kuyafikiliza makusudi yako kwa utukufu wa wana wa Israeli na fahari ya Yerusalemu.

9Akamwabudu Mungu, akawaambia, Waamuru wanifungulie mlango wa mji, nami nitatoka kuyafanya yale tuliyoyasema. Wakawaamuru vijana wamfungulie kama aliyosema; wakafungua.

10Yudithi akatoka, yeye na mjakazi wake, na macho ya watu wa mji yalimfuata aliposhuka milimani na kupitia bondeni, hata wasiweze kumwona tena.

Yudithi atekwa

11Wakashika njia moja kwa moja bondeni; walinzi wa Waashuri wakakutana naye,

12wakamshika, wakamwuliza, Mtu gani wewe? Unatoka wapi, na kwenda wapi? Akasema, Mimi ni binti wa Waebrania, nami ninatoroka kwao, kwa sababu wa karibu kutolewa kwenu na kuangamizwa.

13Basi, ninamwendea Holofene, jemadari mkuu wa jeshi lenu, kumpa maneno ya kweli na kumwonesha njia atakayoweza kuifuata ili ajipatie nchi yote ya milima bila kupoteza hata mtu mmoja au maisha yake.

14Basi, wale watu walipoyasikia maneno yake, na kutazama sura yake, ambayo uzuri wake uliwashangaza,

15walimwambia, Umejiokoa nafsi yako kwa kumjia bwana wetu; basi, sasa twende nyumbani kwake; wengine wetu watakupeleka hata kukuweka mikononi mwake.

16Nawe utakaposimama mbele yake, usiwe na hofu moyoni mwako, bali umweleze maneno yako hayo, naye atakutendea mema.

17Wakachagua watu mia moja miongoni mwao wakawaagiza wamsindikize, pamoja na mjakazi wake, wakawaleta hemani kwa Holofene.

18Watu wa kambini mwote wakakusanyika, maana habari za kuja kwake zilienea mahemani; wakaja wakamzunguka pale aliposimama nje ya hema ya Holofene, watu walipokuwa wakimweleza habari zake.

19Wakaustaajabia uzuri wake, na kuwastaajabia wana wa Israeli kwa ajili yake. Wakasemezana kila mtu na jirani yake, Nani awezaye kuwadharau watu hawa, madhali miongoni mwao mna wanawake wazuri kama huyu! Haifai waachwe, hata mtu mmoja, maana wakiachwa wataweza kuushawishi ulimwengu wote.

Yudithi aletwa mbele ya Holofene

20Basi, wale waliomhudumia Holofene, na watumishi wake wote, walitoka wakamwingiza hemani.

21Naye Holofene alikuwa akipumzika kitandani chini ya chandarua chake, kilichofumwa kwa urujuani na dhahabu na zamuridi na vito vya thamani.

22Wakamweleza habari zake. Akatoka, akaja uwanjani mbele ya hema yake, na taa za fedha zilimtangulia.

23Hata Yudithi aliposimama mbele yake na watumishi wake, wote waliustaajabia uzuri wa sura yake. Akaanguka kifudifudi akamsujudia; watumishi wake wakamwimua.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya