Yudithi 12

Yudithi 12

Yudithi anakuwa mgeni wa Holofene

1Akaamuru apelekwe mezani vilipowekwa vyombo vyake vya fedha, akaandaliwe chakula katika vyakula vyake yeye, na kupewa mvinyo yake anywe.

2Yudithi akasema, La, sitakula hicho, nisije nikakosa; bali chakula changu kitengenezwe kwa vitu nilivyokuja nayvo.[#Dan 1:8; Estk 4:17w]

3Holofene akamwambia, Lakini kama vile vitu ulivyo navyo vikipungua, tutawezaje kukupatia vingine, madhali kwetu hakuna mtu wa taifa lako?

4Yudithi akamwambia, Bwana wangu, roho yangu iishivyo, mtumishi wako hatavimaliza vile vitu nilivyo navyo hata BWANA atimize kwa mkono wangu yale mambo aliyoyakusudia.

5Watumishi wa Holofene wakampeleka hemani, akalala hata usiku wa manane,

6hata wakati wa alfajiri alituma mtu kwa Holofene kusema, Sasa bwana wangu atoe amri wamruhusu mtumishi wako aondoke akasali.

7Holofene akawaagiza walinzi wake wasimzuie. Akakaa kambini siku tatu, akiondoka kila siku kwenda katika bonde la Bethulia, na kunawa kisimani.

8Alipotoka alimwomba Mungu wa Israeli ainyoshe njia yake apate kuwainua wana wa taifa lake.

9Akarudi ametakasika, akakaa hemani hata alipokula chakula cha jioni.

Yudithi karamuni

10Ikatokea, siku ya nne, Holofene aliwafanyia karamu watumsihi wake mwenyewe tu, wala hakuwaalika maakida wake.

11Akamwambia Bagoa, towashi, aliyekuwa juu ya vitu vyake vyote, nenda sasa, umshawishi yule bibi wa Kiebrania aliyepo kwenu aje kwetu, kula na kunywa pamoja nasi.

12Maana ni aibu kwetu tukimwacha mwanamke kama huyu aondoke bila kuzungumza naye. Na kama tusipomkaribisha kwetu atatudharau.

13Bagoa akatoka mbele ya Holofene, akamwendea, akasema, Msichana mwema asiogope kumjia bwana wangu na kuheshimiwa mbele yake, na kunywa divai na kufurahi pamoja nasi, na kuwa leo kama mmoja wa binti za wana wa Ashuru wanaohudumu katika nyumba ya Nebukadreza.

14Yudithi akamwambia, Nami ni nani nimkatae bwana wangu? Yoyote yapendezayo machoni pake nitayafanya mara; hii itakuwa furaha yangu hata siku ya kufa kwangu.

15Akaondoka, akajipamba kwa mavazi na mapambo yote ya kike; mjakazi wake akaenda akamtandikia ngozi karibu na Holofene, ndizo ngozi alizopewa na Bagoa kwa matumizi yake ya kila siku, ya kulia na kulalia.

16Yudithi akaingia akaketi, moyo wa Holofene ukamfurahia na roho yake ikachochewa, akamwonea shauku sana. Naye, tangu siku ya kwanza aliyomwona, alikuwa akitafuta nafasi ya kumbembeleza.

17Holofene akamwambia, Basi, unywe, ufurahi pamoja nasi.

18Yudithi akasema, Bwana wangu, nitakunywa, maana nafsi yangu imetukuka ndani yangu leo kuliko siku yoyote tangu kuzaliwa kwangu.

19Akatwaa vile vitu vilivyoandaliwa na mjakazi wake, akala na kunywa mbele yake.

20Holofene akamfurahia sana, akanywa divai nyingi mno kuliko alivyokunywa kwa wakati mmoja katika siku yoyote tangu kuzaliwa kwake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya