The chat will start when you send the first message.
1Basi, wale waliokuwamo mahemani waliposikia, walishtukia jambo hili lililotukia.
2Tetemeko na hofu iliwashika, wala hakuna mtu aliyethubutu kukaa tena machoni pa wenzake, ila wote waliporomoka ovyo, wakakimbia huku na huko katika njia za uwandani na milimani.
3Nao pia waliokuwako milimani wakiihusuru Bethulia walikimbia. Wana wa Israeli, kila aliyeweza vita, wakaenda mbio kuwashambulia.
4Uzia akapeleka watu Betomesthaimu na Bebai na Chobai na Chola, na kila mahali katika Israeli, kuwaeleza mambo yaliyofanyizwa, ili wote wawashambulie adui zao na kuwaharibu.
5Basi, wana wa Israeli waliposikia, waliwaangukia kwa nia moja wakawapiga hata Chobai; naam, wakaja pia watu wa Yerusalemu na wa nchi yenye milima (maana watu walikuwa wamewaambia mambo yaliyotokea katika kambi ya adui zao), nao wa Gileadi na Galilaya waliwatokea kandokando wakawa wakiua wengi wao, hata walipopita Dameski na mipaka yake.
6Na wengine, waliokaa Bethulia, waliiangukia kambi ya Ashuru wakaiteka wakapata mali nyingi.
7Nao wana wa Israeli waliporudi baada ya kuwaua waliteka nyara vitu vilivyobaki; na watu wa vijiji na miji ya milimani na ya uwandani waliteka pia, maana kulikuwako vitu vingi sana.
8Yoakimu, kuhani mkuu, na wazee wa baraza ya wana wa Israeli waliokaa Yerusalemu, walikuja kuyaona mambo mema BWANA aliyowatendea Israeli, na kumtazama Yudithi na kumsalimu.
9Nao walipomjia walimbariki kwa moyo mmoja wakamwambia, Wewe ndiwe utukufu wa Israeli, wewe ndiwe fahari ya taifa letu;
10umeyatenda hayo yote kwa mkono wako; umeifanyia mema Israeli, na Mungu amependezwa nayo. Ubarikiwe na BWANA Mwenyezi hata milele. Watu wote wakasema, Amin.
11Watu wakaliteka kambi muda wa siku thelathini. Wakampa Yudithi hema la Holofene, na vikombe vyake vya fedha vyote, na vitanda vyake, na vyombo vyake, na mapambo yote ya hemani mwake. Akavipokea, akavipandisha juu ya nyumbu wake, akayatengeneza magari yake akavipakiza humo.
12Wanawake wote wa Israeli walikusanyika mbio kumtazama; wakambariki, wakamchezea ngoma. Akatwaa matawi akawapa wanawake waliokuwa naye.
13Wakajitia taji za majani ya mizeituni, yeye na wale waliokuwa pamoja naye. Akatangulia mbele ya watu wote katika ngoma akiwaongoza wanawake; na wanaume wote wa Israeli walifuata, wamevaa mavazi ya vita na kujitia taji, na nyimbo vilikuwamo vinywani mwao.
14Yudithi akaanza kuimba wimbo huu wa shukrani katikati ya Waisraeli, na watu wote waliuitikia kwa sauti kubwa: