Yudithi 2

Yudithi 2

Vita juu ya magharibi

1Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane, siku ya ishirini na mbili ya mwezi wa kwanza, kulikuwa na mashauri katika nyumba ya Nebukadreza, mfalme wa Waashuri, kwamba ajilipize kisasi juu ya nchi yote, kama alivyosema.

2Akawaita watumishi wake wote, na wakuu wake wote, akawaeleza azimio lake la siri, akakata shauri kwa kinywa chake mwenyewe kuitesa nchi yote.

3Wakakusudia kuwaharibu wenye mwili wote wasiolifuata neno la kinywa chake.

4Ikawa, alipokuwa ameyamaliza mashauri yake, Nebukadreza alimwita Holofene, jemadari mkuu wa majeshi yake, wa pili baada yake yeye, akamwambia:

5Mfalme mkuu, bwana wa dunia yote, asema hivi: Tazama, utaondoka kwangu, na kujitwalia watu wenye nguvu na ujasiri, askari wa miguu hata elfu mia moja na ishirini, na hesabu ya farasi na wawapandao elfu kumi na mbili;

6nanyi mtatoka kupigana na nchi yote ya magharibi, kwa sababu hawakulitii neno la kinywa changu.

7Nawe utawaonya kwamba waweke tayari ardhi na maji, kwa kuwa nitawatokea katika hasira yangu na kuufunika uso wote wa ardhi kwa miguu ya majeshi yangu, na kuwafanya wao mateka kwao.

8Na maiti zao zitajaza mabonde yao na vijito, na mto utajaa wafu wao hata ufurike;

9nami nitawachukua mateka hata miisho ya dunia.

10Lakini wewe utatangulia na kunitwalia maeneo yao yote, nao watajitoa kwako, nawe utawaweka hata siku nitakayokuja kuwahukumu.

11Bali, kwa habari za wale wasiotii, jicho lako halitawahurumia, ila utawatoa kuuawa na kuangamizwa katika nchi yote.

12Maana, kama niishivyo, na kwa uwezo wa milki yangu, nimenena; nami nitayatekeleza hayo kwa mkono wangu.

13Basi, usiasi amri yoyote ya bwana wako, bali uzitimilize sawasawa kama nilivyokuamuru, wala usikawie.

Juhudi za Holofene za kueneza vita

14Naye Holofene alitoka mbele ya uso wa bwana wake, akawaita wakuu wote wa majemadari na maofisa wa jeshi la Ashuru,

15akahesabu watu hodari wa vita, kama bwana wake alivyomwamuru, hata elfu mia moja na ishirini, na wapiga mishale na farasi wao elfu kumi na mbili;

16akawapanga, kama mkutano mkubwa upangwavyo kwa vita.

17Akachukua ngamia na punda na nyumbu kwa mizigo yao, wengi mno; na kondoo na ng'ombe na mbuzi bila idadi kwa chakula cha njiani,

18na akiba kubwa ya chakula kwa kila mtu; na dhahabu na fedha nyingi sana kutoka katika nyumba ya mfalme.

19Akatoka yeye na jeshi lake lote, wakashika njia kwenda kujionesha kwa mfalme Nebukadreza na kuufunika uso wote wa ardhi upande wa magharibi kwa magari yao na wapanda farasi na askari wateule wa miguu.

20Na watu wengi wa mataifa kadha wa kadha walifuatana nao kama nzige na kama mchanga wa ardhi, yaani hawakuhesabika kwa sababu ya wingi wao.[#Amu 7:12; Yoe 2:2-11]

Vituo vya jeshi la Holofene

21Wakatoka Ninawi safari ya siku tatu kuuendea uwanda wa Bektilethi; na kutoka Bektilethi walipiga kambi karibu na mlima upande wa kushoto wa Kilikia ya juu.

22Akalichukua jeshi lake lote, askari wa miguu na wa farasi, na magari, akatoka huko akaenda nchi yenye milima,

23akaharibu Putu na Ludu, akaangamiza Bani Rasesi wote na Bani Ishmaeli, ambao walikaa karibu na nyika upande wa kusini wa nchi ya Wacheli.

24Akauvuka mto Frati, akapitia Mesopotamia, akaiharibu miji yote ya juu iliyokuwako kando ya mto Abonai hata ufike baharini.

25Akajichukulia nchi ya Kilikia akawaua watu waliompinga, akafika kwenye mipaka ya Yafethi, upande wa kusini karibu na Arabuni.

26Akawazunguka Bani Midiani pande zote, akayachoma moto mahema yao na kuyateka mazizi ya kondoo.

27Akaushukia uwanda wa Dameski wakati wa mavuno ya ngano, akayatia moto mashamba yao yote, akayaharibu kabisa makundi yao; akaiteka miji yao na kuuacha uwanda wao ukiwa; akawaua vijana wao wote kwa upanga.

28Basi, kwa ajili yake hofu na woga viliwaangukia wote waliokaa pwani ya bahari, nao waliokuwako Sidoni na Tiro, na waliokaa katika Suru na Osina; na watu waliokaa katika Azota na Ashkeloni wakamwogopa mno.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya