Yudithi 6

Yudithi 6

Akioro atolewa kwa Waisraeli

1Basi ghasia ya wale watu waliokuwako barazani ilipotulia, Holofene, jemadari mkuu wa jeshi la Ashuru, alisema na Akioro na wana wote wa Amoni, mbele ya wageni wote, akawaambia:

2U nani wewe, Akioro; nanyi watu wa mshahara wa Efraimu; hata unafanya unabii katikati yetu, kama leo, na kusema tusifanye vita na Waisraeli kwa sababu Mungu wao atawalinda? Ni nani aliye Mungu ila Nebukadreza? Yeye atatia uwezo wake na kuwafuta katika uso wa nchi, na Mungu wao hatawaokoa;

3ila sisi, watumishi wake, tutawapiga kwa umoja, wasiweze kuistahimili nguvu ya farasi zetu.

4Maana kwa hao tutawateketeza, hata milima yao italevywa kwa damu yao, na mabonde yao yatajazwa kwa mizoga yao; hatua zao hazitaonekana tena mbele yetu, maana hakika watapotea, asema Nebukadreza, bwana wa dunia yote. Na maneno aliyoyasema hayatakuwa bure.

5Lakini wewe, Akioro, mtu wa mshahara wa Amoni, uliyesema maneno hayo siku ya uovu wako, hutaniona uso tena tangu leo hata nijilipize kisasi juu ya ukoo wa wale waliotoka Misri.

6Ndipo upanga wa askari zangu, na wale wengi waliopo upande wangu, utakuchoma mbavuni, nawe utaanguka katikati ya wafu wao, nitakaporudi.

7Basi, watumishi wangu watakupeleka katika nchi yenye milima na kukuacha katika mji mmojawapo katika njia za kupandia,

8usife mpaka utakapoangamia pamoja nayo.

9Basi, kama ukiamini moyoni mwako ya kuwa hawatashindwa, mbona uso wako unaonesha hofu? Haya! Nimesema, wala hakuna neno langu hata moja litakaloanguka chini.

10Holofene akawaamuru watumwa wake waliohudumu hemani mwake wamshike Akioro na kumpeleka Bethulia na kumtia katika mikono ya wana wa Israeli.

11Watumwa wake wakamtwaa wakamtoa kambini na kumpeleka uwandani, kisha walitoka uwandani wakaenda milimani wakafika kwenye visima chini ya Bethulia.

12Watu wa mjini walipowaona juu ya milima walishika silaha zao wakatoka mjini kupigana nao; kila mtu mwenye kombeo waliwatupia mawe na kuwazuia wasipande.

13Wakarejea nyuma kwa siri wakafika chini ya mlima, wakamfunga Akioro, wakamwangusha chini wakamwacha huko, wakamrudia bwana wao.

14Wana wa Israeli wakashuka kutoka mjini mwao, wakamkuta, wakamfungua wakampeleka Bethulia, wakamweka mbele ya wakuu wa mji.

15Nao wakuu wakati ule walikuwa Uzia, mwana wa Mika, wa kabila ya Simeoni, na Chabrisi, mwana wa Gothonieli, na Charmisi, mwana wa Melkieli.

16Wakawaita wazee wa mji wote; na vijana wao wote walikusangika mbio, na wanawake pia, kwenye baraza. Wakamweka Akioro katikati ya watu wao wote.

17Uzia akamwuliza habari zake, naye akajibu, akawaeleza mashauri yote ya baraza ya Holofene, na maneno yote aliyoyasema katikati ya wakuu wa wana wa Ahuru, na majivuno yake Holofene juu ya nyumba ya Israeli.

18Watu wakaanguka wakamsujudia Mungu, wakamwomba wakisema:

19Ee BWANA, Mungu wa mbinguni, tazama kiburi chao, uhurumie unyonge wa taifa letu, uwatazame uso wale waliotakasika kwako leo.

20Wakamfariji Akioro wakamsifu sana.

21Uzia akampeleka nyumbani kwake kutoka barazani, akawafanyia wakuu karamu; wakamlilia Mungu wa Israeli usiku kucha wakimwomba msaada.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya