The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA lililomjia Yeremia, kuhusu ukosefu wa mvua.
2Yuda huomboleza,[#Isa 3:26; 15:3,4; Kut 11:6; Mit 21:13]
Na malango yake yamelegea;
Wameketi chini wamevaa kaniki;
Na kilio cha Yerusalemu kimepaa juu.
3Na wakuu wao huwatuma watoto wao kwenye maji;[#Zab 40:14; 2 Sam 15:30]
Nao hufika visimani wasipate maji;
Hurudi, na vyombo vyao ni vitupu;
Wametahayarika na kufadhaika,
Na kuvifunika vichwa vyao.
4Kwa sababu ya nchi iliyopasuka,
Kwa kuwa mvua haikunyesha katika nchi,
Wakulima wametahayarika,
Na kuvifunika vichwa vyao.
5Naam, kulungu naye uwandani amezaa,
Akamwacha mwanawe kwa kuwa hakuna majani.
6Na punda mwitu husimama juu ya vilele vya milima,[#Yer 2:24]
Hutwetea pumzi kama mbwamwitu;
Macho yao hayaoni sawasawa,
Kwa kuwa hapana majani.
7Ijapokuwa maovu yetu yanatushuhudia, lakini utende wewe kwa ajili ya jina lako, Ee BWANA, maana kurudi nyuma kwetu ni kwingi; tumekutenda dhambi.[#Zab 25:11]
8Wewe uliye tumaini la Israeli, wewe uliye Mwokozi wake wakati wa taabu, kwa nini wewe umekuwa kama mtu akaaye katika nchi, kama mgeni, na kama mtu mwenye kusafiri, ageukaye upande ili kukaa usiku mmoja tu?[#Yer 17:13; Mdo 28:20; 1 Tim 1:1; Zab 46:1]
9Kwa nini wewe umekuwa kama mtu aliyeshtuka, kama shujaa asiyeweza kuokoa? Lakini wewe, BWANA, u katikati yetu, nasi tunaitwa kwa jina lako; usituache.[#Isa 59:1; Kut 29:45]
10BWANA awaambia watu hawa hivi, Hivyo ndivyo walivyopenda kutangatanga; hawakuizuia miguu yao; basi, BWANA hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, atawapatiliza dhambi zao.[#1 Fal 17:18; Zab 109:14; Hos 8:13; Ebr 8:12]
11Naye BWANA akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.[#Kut 32:10]
12Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.[#Mit 1:28; Isa 1:15; Yer 11:11; Mik 3:4]
13Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.
14Ndipo BWANA akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao.[#Isa 30:10; Yer 23:21; 2 The 2:9-11]
15Basi, kwa hiyo BWANA asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, lakini husema, Upanga na njaa havitaingia katika nchi hii; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa.[#Yer 23:15]
16Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao.[#Mt 15:14; Zab 79:3]
17Nawe utawaambia neno hili, Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha lisiloponyeka.[#Omb 1:16; Yer 8:21]
18Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huku na huko katika nchi, wala hawana maarifa.[#Eze 7:15]
19Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yoyote, tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu![#2 Fal 17:20; Zab 78:59; Omb 5:22]
20Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi.[#Ezr 9:5; 1 Yoh 1:9; Dan 9:8]
21Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako, kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi.[#Yer 17:12]
22Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, Ee BWANA, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.[#Isa 30:23]