The chat will start when you send the first message.
1Tena neno la BWANA likanijia, kusema,
2Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa.[#Mwa 19:14]
3Maana BWANA asema hivi, kuhusu habari za wana, na kuhusu habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na kuhusu habari za mama zao waliowazaa, na kuhusu habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii;
4watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.
5Maana BWANA asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema BWANA, hata fadhili zangu na rehema zangu.[#Zab 78:64; Eze 24:17]
6Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikatakata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao;[#Kum 14:1; Isa 22:12]
7wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao.[#Mit 3:6]
8Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa.
9Maana BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.[#Isa 24:7; Hos 2:11; Yer 7:34; 25:10; Ufu 18:23]
10Tena itakuwa, utakapowaonesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, Mbona BWANA amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda BWANA, Mungu wetu, ni nini?[#Kum 29:24; Yer 5:19; 13:22]
11Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema BWANA, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;[#Amu 2:12,13; 1 Fal 9:9; 2 Nya 7:22; Neh 9:26-29; Zab 106:35-41; Yer 5:7,9; Dan 9:10-12]
12na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;[#Yer 7:26; 2 Tim 3:13]
13basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.[#Law 18:27,28; Kum 4:26; 2 Nya 7:20; Yer 15:4]
14Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
15lakini, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao.
16Tazama, asema BWANA, Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali.[#Amo 4:2; Hab 1:15]
17Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote, hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu yasiuone.[#Ayu 34:21; Mit 5:21; Yer 32:19]
18Nami kwanza nitawalipa uovu wao na dhambi zao maradufu, kwa kuwa wameitia unajisi nchi yangu, kwa mizoga ya vitu vyao vichukizavyo, na kuujaza urithi wangu kwa machukizo yao.[#Mik 4:10; Eze 43:7]
19Ee BWANA, nguvu zangu, ngome yangu, na kimbilio langu siku ya taabu, kwako wewe watakuja mataifa yote toka ncha za dunia, wakisema, Baba zenu hawakurithi kitu ila uongo, naam, ubatili na vitu visivyofaa.[#Zab 18:2; 22:27; Isa 2:2; 44:10]
20Je! Mwanadamu ajifanyie miungu, wasio miungu?[#Isa 37:19; Gal 4:8]
21Basi, tazama, nitawajulisha, mara moja hii nitawajulisha, mkono wangu, na nguvu zangu; nao watajua ya kuwa, jina langu ni YEHOVA.