The chat will start when you send the first message.
1Dhambi ya Yuda imeandikwa kwa kalamu ya chuma, na kwa ncha ya almasi; imechorwa katika kibao cha moyo wao, na katika pembe za madhabahu zenu;[#Ayu 19:24; Mit 3:3; 2 Kor 3:3]
2na wakati huo watoto wao wazikumbuka madhabahu zao, na maashera yao, karibu na miti yenye majani mabichi juu ya milima mirefu.[#2 Fal 16:4; 2 Nya 24:18; Isa 1:29]
3Ee mlima wangu wa uwandani, nitatoa mali zako na hazina zako zote ziwe nyara, na mahali pako palipoinuka, kwa sababu ya dhambi, katika mipaka yako yote.[#Yer 15:13]
4Nawe, naam, wewe nafsi yako, utaachana na urithi wako niliokupa; nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana umewasha moto katika hasira yangu, utakaowaka milele.[#Yer 16:13]
5BWANA asema hivi,[#Isa 30:1]
Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu,
Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake
Na moyoni mwake amemwacha BWANA.
6Maana atakuwa kama fukara nyikani,[#Ayu 20:17]
Hataona yatakapotokea mema;
Bali atakaa jangwani palipo ukame,
Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.
7Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA,[#Zab 2:12; Mit 16:20]
Ambaye BWANA ni tumaini lake.
8Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji,[#Zab 1:3]
Uenezao mizizi yake karibu na mto;
Hautaona hofu wakati wa joto ujapo,
Bali jani lake litakuwa bichi;
Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua,
Wala hautaacha kuzaa matunda.
9Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?[#Mwa 6:5]
10Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.[#1 Sam 16:7; 1 Nya 28:9; Zab 7:9; 139:23; 62:12; Yer 11:20; 20:12; 32:19; Mit 17:3; Rum 8:27; 2:6; Ufu 2:23]
11Kama kware akusanyaye makinda asiyoyaangua, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya maisha yake itamtoka, na mwisho wake atakuwa mpumbavu.[#Lk 12:20]
12Kiti cha enzi, cha utukufu, kilichowekwa juu tangu mwanzo, ndicho mahali patakatifu petu.
13Ee BWANA, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha BWANA, kisima cha maji yaliyo hai.[#Zab 73:27; Yer 2:26; Isa 1:28; 65:13; Eze 16:63; 36:32; Dan 12:2; Lk 10:20]
14Uniponye, Ee BWANA, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.
15Tazama, wao waniambia, Neno la BWANA liko wapi? Na lije, basi.[#Isa 5:19; Eze 12:22; Amo 5:18; 2 Pet 3:4]
16Mimi hapa sikufanya haraka kuacha kuwa mchungaji nyuma yako; wala sikuitamani siku ya maradhi ya kuua; wewe unajua; yaliyotoka midomoni mwangu yalikuwa mbele za uso wako.
17Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi; wewe ndiwe uliye kimbilio langu siku ya uovu.
18Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.
19BWANA akaniambia hivi, Nenda ukasimame katika lango la wana wa watu hawa, waingiapo wafalme wa Yuda, na watokeapo, na katika malango yote ya Yerusalemu,
20ukawaambie, Lisikieni neno la BWANA, enyi wafalme wa Yuda, na Yuda wote, nanyi wenyeji wote wa Yerusalemu, ninyi mwingiao kwa malango haya;[#Zab 49:1; Yer 19:3; 22:2; Eze 2:7; 3:17; Hos 5:1; Mik 3:1]
21BWANA asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wowote siku ya sabato, wala msiulete ndani kwa malango ya Yerusalemu;[#Hes 15:32; Neh 13:15-22]
22wala msitoe mzigo katika nyumba zenu siku ya sabato, wala msifanye kazi yoyote; bali itakaseni siku ya sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu;[#Kut 20:8-10; 23:12; 31:13; Eze 20:12; Kum 5:12-14]
23lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, ili wasisikilize wala wasipokee mafundisho.
24Na itakuwa, kama mkinisikiliza mimi kwa bidii, asema BWANA, msiingize mzigo wowote katika mlango wa mji huu siku ya sabato, bali muitakase siku ya sabato, bila kufanya kazi yoyote siku hiyo;
25ndipo watakapoingia wafalme na wakuu kwa malango ya mji huu; wataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kupanda magari na farasi, wao, na wakuu wao, watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; na mji huu utakaa hata milele.[#Kum 4:40]
26Nao watatoka miji ya Yuda, na mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na nchi ya Benyamini, na Shefela, na milima, na upande wa Negebu, wakileta sadaka za kuteketezwa, na dhabihu, na sadaka za unga, na ubani, wakileta pia sadaka za shukrani, nyumbani kwa BWANA[#Zek 7:7; Zab 107:22; #17:26 tafsiri yake ni Nchi ya mabonde.; #17:26 tafsiri yake ni Nchi ya kusini.]
27Lakini kama hamtaki kunisikiliza, kuitakasa siku ya sabato, kutokuchukua mzigo katika malango ya Yerusalemu siku ya sabato; basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utaziteketeza nyumba za enzi za Yerusalemu, wala hautazimika.[#Omb 4:11; Amo 1:4; 2 Fal 25:9]